*************************
Na John Walter-Babati
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Babati mkoa wa Manyara kimefanya tafrija ya kumuaga aliyekuwa Katibu wa chama hicho Daniel Muhina baada ya kuhamishwa kikazi kutoka mkoani hapa kwenda mkoani Kagera.
Wanachama hao Wilaya ya Babati, wafanyabiashara na wadau mbalimbali wamemuaga Katibu huyo wa Babati Mjini Daniel Muhina aliyehamishiwa wilayani Bukoba Mjini Mkoa wa Kagera kwa majukumu kama hayo ndani ya Chama, hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Kisora Usiku wa kuamkia leo Desemba 11,2022.
Wanachama hao wamemtakia kila la kheri Muhina huko aendako, wakimshukuru Kwa utekelezaji wake uliotukuka.
Muhina amesema amefanya kazi ya kuwatetea waliokuwa na Mazingira magumu ndani ya Chama jambo ambalo halikuwapendeza wengine, ikiwa ni pamoja na kufanikisha ajira ya kudumu kwa sekretari wa Chama aliyekuwa akijitolea kwa muda pamoja na kutengeneza Mazingira mazuri ya kuanzia ujenzi wa nyumba ya dereva wa Chama.
Muhina anaeleza alipoona Mazingira ya uonevu ndani ya chama alisimama mstari wa mbele kuwatetea huku wengine bila kuwataja majina yao wakimpinga.
Amewaachia ujumbe wanachama wa CCM kupendana huku akiwakumbusha kuwa kuna leo na kesho.
Akizungumza kwa Niaba ya Mkurugenzi wa Mati super Brand Ltd, meneja ugavi na ununuzi Aikande Lema, amesema kipindi chote walishirikiana kwa karibu na katibu huyo kufanikisha masuala mbalimbali.
Mbunge wa zamani wa jimbo la Babati Vijijini na mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM mkoa Vrajlal Jitusoni amesema kazi ya chama hicho ni Kubwa kwa Wananchi na kina uhakika wa kuchukua Dola mwaka 2025.
Muhina amehudumu kama Katibu mkuu CCM Manyara tangu mwaka 2021 Hadi mwaka 2022 akikisimamia Chama hicho na serikali kutekeleza ilani iliyopo.
Amehamia katika Mji wa Bukoba ambapo hapakuwa na katibu kwa miezi miwili huku Babati Mjini pakiwa wazi kwa zaidi ya miezi miwili na hakuna alietangazwa kuziba nafasi hiyo.
Hata hivyo tukio hilo pia limehudhuriwa na Katibu Tawala Wilaya ya Babati Khalfan Mathipula ambaye amesema Muhina alikuwa ni daraja zuri kati ya chama na Serikali.