Alisema kukamilika kwa mradi huo kunaifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza kusimika huduma za mawasiliano katika kilele cha Mlima kilimanjaro, jambo ambalo litaongeza kasi ya kuutangaza mlima huo duniani na kuvutia idadi kubwa ya watalii kuutembelea.
“Leo ni siku muhimu kwa Shirika letu la TTCL na Tanzania tunapokwenda kushuhudia tukio la kihistoria la uzinduzi wa intaneti katika kilele cha Mlima Kilimanjaro, utakaofanyika pia rasmi kwenye kileleni cha mlima Desemba 13, 2022 tukiwa huko kileleni,” alisema Mhe. Nnauye.
Jumla ya kilometa 44.7 za njia ya Mkongo wa Mawasiliano zimejengwa kuanzia Kituo cha Marangu hadi kwenye kilele cha Mlima Kilimanjaro, uwekezaji ambao umefanikisha vituo vyote vilivyopo katika Mlima Kilimanjaro kupata mawasiliano ya intaneti na simu za mezani.
“Tangu kuzinduliwa kwa huduma za mawasiliano katika vituo vya awali, watalii wanaopanda mlimani wameanza kuzungumza na ndugu, jamaa na marafiki wakiwa mlimani na kuelezea uzuri wa vivutio vyetu jambo ambalo linaendelea kuutangaza utalii nchini, licha ya kurahisisha shughuli za huduma kwa watalii zinazofanywa na taasisi mbalimbali katika Mlima Kilimanjaro,” alisisitiza Waziri Nnauye.
Awali akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Eng. Peter Ulanga alisema uwepo wa huduma hiyo ya mawasiliano katika Mlima Kilimanjaro itaboresha upatikanaji wa huduma za afya kwa watalii mlimani, pia wanapopata dharura yoyote wakiwa safarini.
Aidha aliongeza uwepo wa huduma za mawasiliano utaimarisha shughuli za ulinzi na usalama kwa watalii wakiwa mlimani kupitia mamlaka husika jambo ambalo ni kivutio cha kuchocheza na kuvutia watalii wengi kuutembelea.
“Mkakati wa Shirika wa miaka mitano ni kuhakikisha huduma za mkongo zinawafikia wananchi katika makazi yao, maeneo ya biashara, maofisini na sehemu za vivutio vya utalii wetu, TTCL inatambua umuhimu wa utalii nchini hivyo tutaongeza nguvu kutoa huduma za mawasiliano kupitia mkongo katika maeneo mengine ya utalii ili kuchochea shughuli za utalii nchini,” alibainisha Eng. Ulanga.