Na Mathias Canal, WEST-Dodoma
Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia imesema haina sababu ya kuagiza Vishikwambi kutoka nje ya nchi
itaunga mkono jitihada za kampuni yoyote yenye nia ya kuanzisha kiwanda cha
utengenezaji wa vishikwambi nchini.
Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda amesema hayo Jijini Dodoma wakati alipokutana
na Ndg Tosk Hans ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya TANZTECH ELECTRONICS
LIMITED ya Jijini Arusha ambayo imedhamiria kuanza uzalishaji wa vishikwambi
ndani ya nchi kwa ajili ya matumizi ya wanafunzi.
Kampuni hiyo tayari ina eneo
Jijini Arusha kwa ajili ya kuanza uzalishaji wa vishikwambi na wataanza
uzalishaji wa baadhi ya vifaa kama vile betri, na Cover huku wakiwa na program
ya kuanza kuwafundisha watanzania mambo ya Uhandisi Electroniki.
Waziri Mkenda amesema kuwa
kampuni yoyote itakayokuja nchini na utaratibu na masharti hayo aliyoyaweka
ambayo ni kampuni kuanzisha Programu ya haraka ya baadhi ya vifaa kuanza
kuunganishwa na kuzalishwa hapa nchini pia kampuni kuandaa programu ya
kufundisha wanafunzi uhandisi Elekroniki, basi Wizara ya Elimu, Sayansi na
Teknolojia itaunga mkono na kuipa kazi kwa ajili ya ununuzi wa vifaa hivyo.
“Tukipata kampuni kama hii
ambayo itaanzisha uzalishaji wa Tablets nchini basi tutaacha kuagiza nje badala
yake tutanunua kwao” Amesisitiza Waziri Mkenda
Pamoja na masharti hayo pia
amesema kuwa masharti mengine ya msingi yatakayofanya Wizara yake kununua
vishikwambi hivyo ni pamoja na ubora wa vishikwambi sambamba na bei rafiki
kuliko kampuni zingine katika soko la Dunia.
Waziri Mkenda amesema kuwa
hakutakuwa na upendeleo wowote kwa wale wanaotaka kuanzisha kuuza vishikwambi
serikalini badala yake kampuni zenye uhitaji huo ni lazima zifuate masharti
hayo aliyoyaweka.
Sambamba na hayo, Waziri
Mkenda ameipongeza kampuni hiyo ya TANZTECH ELECTRONICS LIMITED kwa kukubali
kufuata masharti ya Wizara ya Elimu iliyoyaweka kuanzisha kiwanda cha
utengenezaji wa vishikwambi nchini.