NAIBU Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dk.Charles Msonde,akizungumza wakati akifunga mkutano wa mwaka wa tathmini ya maendeleo ya sekta ya elimu uliojumuisha wadau wa elimu na washirika wa maendeleo uliofanyika kwa siku mbili jijini Dodoma.
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. James Mdoe,akizungumza wakati wa Mkutano wa mwaka wa tathmini ya maendeleo ya sekta ya elimu uliojumuisha wadau wa elimu na washirika wa maendeleo uliofanyika kwa siku mbili jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Caroline Nombo,akizungumza wakati wa Mkutano wa mwaka wa tathmini ya maendeleo ya sekta ya elimu uliojumuisha wadau wa elimu na washirika wa maendeleo uliofanyika kwa siku mbili jijini Dodoma.
BAADHI ya washiriki wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dk.Charles Msonde,akizungumza wakati akifunga mkutano wa mwaka wa tathmini ya maendeleo ya sekta ya elimu uliojumuisha wadau wa elimu na washirika wa maendeleo uliofanyika kwa siku mbili jijini Dodoma.
…………………………
Na Alex Sonna-DODOMA
SERIKALI kupitia Mradi wa kuboresha elimu ya sekondari(SEQUIP) inatarajia kujenga shule za Sekondari 1,026 nchini katika kipindi cha miaka mitano.
Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Dk.Charles Msonde wakati akifunga mkutano wa mwaka wa tathmini ya maendeleo ya sekta ya elimu uliojumuisha wadau wa elimu na washirika wa maendeleo.
Dkt.Msonde amesema,kazi hiyo tayari imeanza katika mwaka wa fedha wa wa 2021/22 ambapo shule 232 za kata zinajengwa ili kuwapunguzia wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata shule.
”Katika mwaka wa fedha uliopita Serikali imejenga shule 232 na pia imetoa Sh. bilioni tatu kwa kujenga shule za bweni za wasichana za mkoa kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita ambazo shule 10 zimeanza kujengwa”amesema Dkt.Msonde
“Ni malengo ya serikali kuhakikisha kwamba katika miaka mitano ijayo shule hizi 1,026 ziweze kujengwa nchini na mwaka huu wa fedha serikali inategemea kujenga shule za aina hiyo 184 ambapo shule moja itajengwa katika Halmashauri hapa nchini.”amesema Dkt.Msonde
Hata hivyo amesema kuwa mikakati mingine ya Serikali ni pamoja na kurekebisha Miundombinu katika shule za msingi na sekondari ikiwa ni pamoja na kurekebisha majengo yaliyochakaa au kubomoa na kujenga upya .
“Tunafahamu kwamba kupitia mafanikio ya elimu bila malipo kumekuwa na ongezeko kubwa katika uandikishaji wa wanafunzi katika shule za msingi na kidato cha kwanza katika shule za sekondari ,hii imesababisha uwepo wa wanafunzi wengi madarasani ,lakini Serikali imeamua kwa makusudi kupitia mradi wa ‘Boost’ katika miaka mitano ijayo kuanzia mwaka huu kuhakikisha kwamba hali hii inaondoshwa.”ameeleza
Aidha amesema kuwa Shule za Msingi 17,000 nchini zilizofanyiwa tathmini na serikali kati hizo shule 7,000 zimebainika kuhitaji ukarabati mkubwa kutokana na uchakavu wa miundombinu uliopo.
“Kati ya hizo shule 17,000, shule 7,000 zinahitaji ukarabati mkubwa.Lakini pia tumefanya tathimini kuangalia msongamano kwenye shule zetu na tumebaini kuna shule ambazo zina msongamano mkubwa sana wa wanafunzi,”amesema Dk.Msonde
Amesema serikali imepanga katika mwaka 2022/23 kujenga shule mpya na madarasa zaidi ya 9000 na kwa miaka ijayo wataendelea na mradi wa ujenzi wa shule mpya na ukarabati wa shule.
Kwa upande wake Mratibu wa Elimu wa Tanzania (TENMET), Ochola Wayoga aliishauri serikali kuongeza bajeti ya elimu hadi kufikia asilimia 20 ya bajeti yote ya Serikali ili kusaidia mageuzi ya elimu yanayofanyika hivi sasa ikiwamo kuboresha ubora wa walimu.
Awali, Naibu Katibu wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. James Mdoe ,amewahakikisha wadau kuwa serikali bado imeweka milango wazi ya kupokea maoni ya kina katika kuboresha mapitio ya sera na mitaala.