MKUU wa kitengo cha kodi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Denis Masami,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Desemba 6,2022 jijini Dodoma kuhusu kuwachukulia hatua wananchi ambao hawatalipa malimbikizo ya kodi ya pango la ardhi mara baada ya kuisha kwa kipindi cha msamaha kilichotolewa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Mratibu wa Kodi Mkoa wa Dodoma, Letare Shoo,akielezea hali ya ulipaji kodi ya Pango la Ardhi katika Mkoa wa Dodoma
…………………………..
Na Alex Sonna-DODOMA
SERIKALI Kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imetangaza kuwachukulia hatua wananchi ambao hawatalipa malimbikizo ya kodi ya pango la ardhi mara baada ya kuisha kwa kipindi cha msamaha kilichotolewa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Kauli hiyo imetolewa Leo Desemba 6,2022 jijini Dodoma na Mkuu wa kitengo cha kodi wa Wizara hiyo, Denis Masami wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema umebaki mwezi mmoja kukamilika kwa kipindi hicho cha msamaha.
Amesema kuwa Waziri mwenye dhamana alitangaza uwepo wa msamaha wa malimbikizo ya kodi ya pango la ardhi uliotolewa na na Rais Dk. Samia kwa wananchi wote waliokuwa na madeni ya malimbikizo ya kodi ya pango la ardhi walipe deni la msingi ili wasamehewe riba
Amesema kuwa hatua hizo ni pamoja na kuwapeleka mahakamani, kunadi mali ili kufidia kodi husika na kubatilisha miliki ambapo zitafutwa ili zirudi kwa Rais wapewe watu wengine wenye uwezo wa kuzilipia na kuziendeleza.
”Msamaha huo ulianza Julai hadi Desemba ambapo kwa muda wa miezi mitano wananchi takribani 10,000 wamejitokeza na kunufaika na msahama huo na wamelipa deni la msingi.”amesema Bw.Masami
Amesema kuwa wapo wamiliki milioni mbili wa vipande vya ardhi ambao wapo kwenye mifumo ya wizara na kwamba mwamko wa ulipaji malimbikizo hayo umeongezeka kutoka asilimia 40 hadi asilimia 60 ya ulipaji.
Aidha ametoa wito kwa wananchi kwamba muda uliowekwa na kutangazwa na serikali nafuu ya msamaha iliyotolewa na DK Samia sasa inakaribia kuisha hivyo watumie fursa hiyo kulipa.
“Sasa umebaki mwezi mmoja huu wa Desemba kwamba wananchi wote ambao hawajatumia fursa hii wajitokeze walipe madeni ya msingi ili wasamehewe riba ,”ameeleza
Kwa upande wake Mratibu wa Kodi Mkoa wa Dodoma, Letare Shoo amesema kodi ya pango la ardhi huwa inachajiwa kila mwaka kuanzia Julai hadi Desemba bila adhabu ambapo ifikapo Januari huchajiwa ambao hawakufanya hivyo.
“Muda uliobaki ni mfupi wananchi wengi wanadaiwa kodi ya pango la ardhi kwa kipindi kirefu hivyo watumie muda huu uliotolewa na Rais Samia maana baada ya hapo ambao bado watachukuliwa hatua,”amesisitiza Shoo.