SHIRIKA la Empower Society Transform Lives (ESTL) linalojihusisha na
masuala ya kupinga ukatili wa kijinsia katika muktadha wa dhana hasi ya
kuondokana na vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto kwa ufadhili wa Shirika la Foundation Civil Society (FCS) limetoa mafunzo ya kuwajenge uwezo watu wenye
ulemavu ili waweze kutoa taarifa pale wanapofanyiwa ukatili.
Mafunzo mengine yaliyotolewa ni pamoja dhana
ya ujinsia na ukatili wa kijinsia na aina nyingine za ukatili wa kijinsia
zinazoripotiwa katika kata,vijiji,mitaa,sheria na mikataba mbalimbali ya
kimataifa kuhusu dhana ya ukatili wa kijinsia na ukeketaji.
Pia mafunzo mengine yaliyotolewa ni
fursa za kijasiriamali toka halmashauri, miongozo ya upatikanaji wa mikopo,mfumo
wa upatikanaji wa mkopo wa halmashauri hasa asilimia mbili ya fedha za mkopo
inayotolewa kwa kundi la watu wenye ulemavu mafunzo yaliyotolewa na Afisa
Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Mkoa wa Singida, Shukrani Mbago.
Katika mafunzo hayo Mbago alitoa wito
kwa jamii hasa wazazi kuhakikisha
wanawalinda watoto wao dhidi ya ukatili kwa kuripoti vitendo vya ukatili
sehemu husika ili wanaotenda vitendo hivyo waweze kuchukuliwa hatua.
Afisa Mawasiliano na Vijana wa ESTL,
Edna Mtui alitoa mafunzo yaliohusu dhana ya mila potofu na ndoa za utotoni,
ndoa za kulazimishwa, na athari zake, dhana ya ukeketaji na athari zake na usafirishaji
haramu wa binadamu.
Mtui alisema kwa sasa kuna vitendo vingi vya ukatili wa kijinsia katika
jamii ambao upo wa aina tano ukiwepo ukatili wa kiuchumi ambao wakina mama wanaupitia hasa pale baba
anapouza mazao yote licha ya mama kushiriki katika uzalishaji.
Aidha Mtui aliongeza kuwa kuna vipigo ambavyo akina mama wengi wanavipata
majumbani na ukatili wa watoto wengi kuachishwa masomo yao ili waweze kuolewa.
Alisema kuna watu wengine wapo wanafanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia
pasipo wao kujua, hivyo elimu ni muhimu kwa jamii ili iweze kutambua vitendo
vyote vya ukatili.
Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Kutokomeza Ukeketaji na Ukatili wa
Kijinsia wa ESTL John Nzungu alisema bado kuna baadhi ya wazazi
wanawaficha watoto wenye ulemavu na kuwakosesha haki yao ya msingi ya kupelekwa
shule.
Nzungu aliongeza kuwa mila na desturi pia bado ni changamoto ambapo watoto
wenye ulemavu hawapelekwi kliniki wakiona ni aibu kuwa na mtoto mwenye
ulemavu, sababu hiyo inasababisha kushindwa kupata huduma za afya.
Mwenyekiti wa Watu wenye Ulemavu
Mkoa wa Singida, Boniphace Kitiku alisema ukatili kwa watu wenye ulemavu ni
mkubwa licha ya kuwepo wadau wengi
wanaoshughulika kutoa elimu ya usawa kwa
watu wote ili watu wa kundi hilo wasifanyiwe ukatili.
Kitiku alitoa wito kwa jamii kuwaona walemavu nao ni watu ambao wanaweza
kuishi pamoja kama Mungu alivyowajaalia lakini bado kuna mitazamo hasi kutoka kwa
baadhi ya watu wakiona walemavu ni mtaji wa kukuza biashara hasa zile kubwa na
kuwatafutia balaa baada ya kudanganywa na waganga wa kienyeji.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameiomba serikali na wadau mbalimbali
kuendelea kutoa elimu ya kupambana na
ukatili wa kijinsia ili kupunguza vitendo hivyo ambavyo bado baadhi ya watu
wanaendelea kuvifanya.
Wamesema kuwa baadhi ya wazazi bado wanashikilia mila na desturi
zilizopitwa na wakati ambazo zinasababisha vitendo hivi kuendelea kufanyika
ikiwa ni pamoja na kusema binti kufanyiwa ukeketaji ni kutolewa mikosi.
Wameongeza kueleza kuwa imani za
kishirikina zinachangia kuwepo kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa
kutafuta utajiri, hali inayosababisha
ubakaji kwa watoto, wazee, wagonjwa wa akili kwa dhana kuwa wakitaka kufanikiwa
ni lazima wafanye hivyo kama wanavyoambiwa na waganga wa kienyeji.Mratibu wa Mradi wa Kutokomeza Ukeketaji na Ukatili wa Kijinsia kutoka Shirika la ESTL John Nzungu (kulia) akizungumza.