Kaimu Mkurugenzi wa elimu msingi Venance Manori (aliesimama) akizungumza kwenye mahafali ya nne ya (DIT) Kampasi ya Mwanza kwa niaba ya Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda
Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Profesa Preksedis Ndomba akitoa hotuba kwenye mahafali ya nne ya taasisi hiyo Kampasi ya Mwanza
Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Dkt Richard Masika akizungumza kwenye mahafali ya nne ya taasisi hiyo Kampasi ya Mwanza
Wahitimu wa Stashahada ya sayansi na teknolojia ya maabala na teknolojia ya bidhaa za ngozi DIT Kampasi ya Mwanza
Baadhi ya wahitimu wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi kwenye mahafali ya nne ya taasisi ya teknolojia Dar es salaam kampasi ya Mwanza
Baadhi ya wahitimu wakirusha kofia juu ikiwa ni ishara ya furaha ya kuhitimu
……………………….
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Wahitimu wa taasisi ya Teknolojia Dar es salaam (DIT) Kampasi ya Mwanza wametakiwa kuitumia elimu waliyoipata Kujiajiri ili waweze kujikwamua kimaisha.
Rai hiyo imetolewa leo Jumatano Disemba 7, 2022 na Kaimu Mkurugenzi wa elimu msingi Venance Manori, aliemuwakilisha Waziri wa elimu,sayansi na teknolojia Profesa Adolfu Mkenda kwenye mahafali ya nne ya DIT Kampasi ya Mwanza yaliyofanyika kwenye uwanja wa taasisi hiyo.
Amesema wahitimu wanatakiwa kuwa na dhamira ya Kujiajiri na kuwa tayari kukabiliana na changamoto mbalimbali hatua itakayowasaidia kufikia malengo yao.
” Ninapenda kuwakumbusha kuwa baada ya kuhitimu masomo yenu mafanikio katika maisha yenu hayatategemea elimu mliyoipata bali yatatokana na namna mtakavyoitumia elimu hiyo, ninafahamu zipo changamoto nyingi katika Kujiajiri lakini jambo la muhimu ni uthubutu kwani penye nia pana njia”, amesema Manori
Aidha, amewakumbusha wahitimu kuwa jamii inamatarajio makubwa kutoka kwao hivyo wanapaswa kuonesha umahiri na kuwa mfano bora mahali pa kazi ili kuwapa moyo wazazi,walimu na walezi.
Kwaupande wake Mkuu wa taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) Prof. Preksedis Ndomba, amesema jumla ya wahitimu ni 64 kati yao wanaume ni 46 wanawake 18.
Amesema katika kundi hilo Kuna wahitimu 39 kutoka Kampasi ya Dar es Salaam ambapo wahitimu 12 ni wa shahada ya kwanza na 27 ni Stashahada ambao hawakuhudhurishwa kwenye awamu ya kwanza ya mahafali yaliyofanyika Disemba 1,2022 katika Kampasi kuu ya Dar es Salaam.
Ndomba ameeleza kuwa wahitimu wa Kampasi ya Mwanza ni 25 ambapo 21 wamehitimu ngazi ya Stashahada ya sayansi na teknolojia ya maabala, huku 4 wakiwa na Stashahada ya teknolojia ya utengenezaji wa bidhaa za ngozi.
Amesema wahitimu hao walidahiliwa na kuanza masomo yao katika mwaka wa masomo 2019/2020 kipindi ambacho taasisi hiyo ilikuwa tayari imebadili mfumo wa utoaji mafunzo wa kutumia muda mwingi darasani na kuwa na mfumo mpya wa kutumia muda mwingi kweye vitendo na ziara za mafunzo viwandani.
” Mfumo huo mpya waufundishaji kwa vitendo umewajengea ujuzi katika kutatua changamoto mbalimbali za kijamii ikiwemo utengenezaji wa vitakasa mikono hususani wakati wa ugonjwa wa Covid-19 na utengenezaji wa viatu vya ngozi ambavyo ni sehemu ya sare za wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari”, amesema Prof Ndomba
Naye Mwenyekiti wa Baraza la DIT Dkt.Richard Masika, amesema mafunzo ya ufundi hukamilika vyema endapo mwanafunzi anaposhiriki mafunzo hayo kwa vitendo Viwandani au katika mnyororo wa uzalishaji.
Amesema utekelezaji wa mafunzo kwa vitendo unakabiliwa na changamoto ya uhaba wa nafasi viwandani.
Akisoma risala kwa niaba ya wahitimu wa DIT Nickson Msai amesema wanaushukuru uongozi wa taasisi kwa namna walivyowaandaa kitaaluma na kijamii hivyo kutokana na elimu waliyoipata wanauwezo wa kufanya kazi kama mafundi sanifu katika maeneo mbalimbali ikiwemo viwandani.