Mkuu wa Wilaya ya Newala, Mhe. Aziza A. Mwangosongo akizungumza na
Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wilayani Newala wakati wa
Maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT)
yaliyofanyika wilayani humo jana na kuwahimiza wananchi kufanya
maandalizi mapema ya kuwanunulia vifaa vya shule watoto waliohitimu
darasa la saba.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akizungumza
na wanachama wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) (hawapo
pichani) wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Wanawake
Tanzania (UWT) yaliyofanyika jana wilayani Newala.
Baadhi ya wanachama wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wilayani
Newala wakimsiliza Mgeni Rasmi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe.
George H. Mkuchika (Mb) wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Umoja wa
Wanawake Tanzania (UWT) yaliyofanyika wilayani humo jana.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akimkabidhi
kadi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mmoja wa wananchi aliyejiunga na
CCM akitokea chama cha upinzani.
*********************************
Na James K. Mwanamyoto, Newala
Wanawake nchini wametakiwa kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali katika
uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika tarehe 24 Novemba,
2019 kwani wana nafasi kubwa katika mchango wa maendeleo ya Taifa.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi
wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) ambaye
alikuwa mgeni rasmi wa Maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Wanawake
Tanzania (UWT) wilayani Newala.
Mhe. Mkuchika amewaasa wanawake nchini, kutotegemea nafasi za upendeleo
walizotengewa na Serikali na badala yake wachukue fomu na kuingia katika
kinyang’anyiro na wanaume kugombea nafasi zilizotangazwa kwa mujibu wa
kanuni zinazosimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
“Serikali ya kijiji ndio inayozungumzia suala la maendeleo ya kijiji, hivyo kijiji
ambacho hakina zahanati, mjumbe mwanamke ni hodari wa kukumbusha ujenzi
wa zahanati kwani anatambua umuhimu wa zahanati”, amefafanua Mhe.
Mkuchika.
Mhe. Mkuchika amesema Serikali inataka wanawake washiriki katika vikao vya
Serikali ya kijiji na mtaa ili wawe chachu ya mafanikio katika vijiji na mitaa, kwani
wananchi katika maeneo hayo wanahitaji kupata huduma bora toka Serikalini.
Mhe. Mkuchika ametoa hamasa kwa kina mama kuwa mstari wa mbele
kuwahimiza akina baba kutekeleza ahadi waliyoitoa ya kuchangia chakula cha
watoto wa shule ili kuwawezesha watoto hao kusoma vizuri pasipo kukabiliwa na
changamoto ya njaa.
Aidha, Mhe. Mkuchika ametumia fursa hiyo kuwaeleza wananchi mafanikio ya
yaliyoletwa na Serikali ya Awamu ya Tano katika sekta ya afya kwa kujenga
hospitali za wilaya nchini.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
tangu aingie madarakani amejenga hospitali nyingi za wilaya kuliko alizozikuta,
kwani amedhamiria ndani ya utawala wake kila wilaya nchini iwe na hospitali
yake na ushahidi wa wazi uko katika Wilaya ya Newala ambayo imenufaika na
ujenzi wa kituo cha afya cha Mpunye na Kitangali”, amesema Mhe. Mkuchika.
Mhe. Mkuchika ameongeza kuwa, kwa upande wa ujenzi wa barabara, mara
baada ya Serikali kuweka lami, wananchi wameweza kusafiri kwa muda mfupi
kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine akitolea mfano wa abiria wanaosafiri kwa
mabasi kutoka Mbinga na Newala kwenda Dar es Salaam wamekuwa wakitumia
siku moja badala ya siku mbili kama ilivyokuwa huko nyuma, halikadhalika na
Kutoka Lindi kwenda Dar es Salaam mabasi yamekuwa yakiondoka asubuhi na
kurudi siku hiyo hiyo.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Newala Mhe. Aziza A. Mwangosongo amempongeza
Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa elimu bure kwa watoto ambao
ndio taifa la kesho na amewataka wazazi wa wanafunzi waliohitimu darasa la
saba wilayani humo kuunga mkono azma ya Mheshimiwa Rais kwa kufanya
maandalizi mapema ya kuwanunulia vifaa vya shule ikiwepo sare za shule
watoto wao ili waweze kunufaika na elimu ya sekondari inayotolewa bure na
Serikali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania
(UWT) ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Bi. Zainabu Msuweta amemshukuru
Mhe. Mkuchika kwa nasaha zake na kuahidi kuwa UWT itazifanyia kazi ili ziweze
kuwa na manufaa kwa wanawake wilayani Newala.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala
Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) amepata mwaliko wa kuwa
Mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Wanawake Tanzania
(UWT) wilayani Newala, wakati akiwa mkoani Mtwara kwenye ziara yake ya
kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma mkoani humo.