Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Wakili Anna Henga akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Kituo hicho leo Desemba 6, 2022 Jijini Dar es Salaam.Afisa Mwandamizi Jinsia, Wanawake na Watoto (LHRC), Bi.Getrude Dyabele akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Kituo hicho leo Desemba 6, 2022 Jijini Dar es Salaam. Afisa Mwandamizi Jinsia, Wanawake na Watoto (LHRC), Bi.Getrude Dyabele akifafanua jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 6, 2022 Jijini Dar es Salaam.
*************************
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimetoa ripoti ya kuwa Ukatili wa Wanawake na Watoto umeonekana kuongezeka ambapo matukio 23,685 ya ukatili dhidi ya wanawake yameripotiwa kwa mwaka 2021 pekee ikiwa ni ongezeko la matukio 2,859 kwa mwaka Mmoja.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 6,2022 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Wakili Anna Henga amesema matukio hayo yamehusisha ukatili wa kimwili, ukatili wa kingono, ukatili wa kisaikolojia, ukatili wa kiuchumi pamoja na ukatili wa kidijitali ambao nao umekuwa ukiwatesa wanawake zaidi.
“Mikoa inayoongoza kwa ukatili dhidi ya wanawake katika ripoti iliyotolewa na Haki za Binadamu ni pamoja na Arusha, Manyara, Lindi, Tanga na Mkoa wa Kipolisi wa Temeke jijini Dar es Salaam”. Amesema Wakili Anna.
Amesema katika taarifa iliyotolewa na Benki ya Dunia inayohusu tathimini ya jinsia nchini Tanzania 40% ya wanawake wa umri wa miaka 15 hadi 49 wamepitia ukatili wa kimwili wakati 17% wamepitia ukatili wa kingono.
“Taarifa hii imeenda mbele kusema kuwa 44% ya wanawake wenye umri wa miaka 15-49 wamepitia ukatili wa kimwili pamoja au ukatili wa kingono kutoka kwa mwenza wao” . Amesema
Aidha amesema ukatili wa wenza umekuwa mkubwa sehemu za vijijini kwa 53% kuliko mijini 45%. Asilimia 30% ya wasichana wanapitia ukatili wa kingono kabla ya kufika umri wa miaka 18 huku 58% ya wanawake na 40% ya wanaume wakiamini kuwa mume ana haki ya kumpiga mke wake kwa sababu zozote.
Hata hivyo amesema katika taarifa ya Jeshi la polisi mwaka 2022 iliripoti matukio 472, 544 kwa mwaka 2018, 487 kwa mwaka 2019, 531 kwa mwaka 2020 na 554 kwa mwaka 2021 ya mauaji ya wanawake kutokana ukatili wa wenza, uchawi na imani za kishirikina, mauaji yasiyo ya wenza mashambulio ya wanawake.