Mrakibu wa Uhamiaji na Msemaji wa idara ya Uhamiaji Tanzania,Paul Mselle akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
********************
Julieth Laizer,Arusha.
Arusha .IDARA ya Uhamiaji Mkoa wa Arusha inamsaka mtu aliyesambaza ( video ) ya uzushi kwenye mitandao ya kijamii ikiwaonyesha raia wa kigeni wakilalamika kukaa muda mrefu bila ya kupata huduma kutoka kwa maofisa wa Uhamiaji katika uwanja wa KIA.
Aidha tukio hilo,lilitokea hivi karibuni katika uwanja wa ndege wa Kimataifa Kilimanjaro (KIA) na kusema kuwa picha hiyo imeleta taharuki kubwa .
Akitoa ufafanuzi huo juu ya tukio hilo,Mrakibu wa Uhamiaji na Msemaji wa Uhamiaji Paul Mselle amesema kuwa,uchunguzi na ufuatiliaji walioufanya wamejiridhisha abiria anayelalamika aliingia nchini kwa ndege ya Shirika la ndege la KLM akitokea Amsterdam Novemba 26 mwaka huu,majira ya saa 2:50 usiku.
“Ndege hii ilikuwa na abiria 317 ambapo abiria 226 walishuka KIA majira ya saa 3:06 usiku na kuanza kupata huduma za kuingia nchini,abiria hawa 226 walihudumiwa kwa dakika 94 ambapo watano walihudumiwa kwa dakika mbili na sekunde 40 kwa kila abiria .”amesema Mselle.
Aidha amesema kuwa, abiria 91 waliokuwa washukie katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) walielekezwa kushuka uwanja wa KIA saa 5:45 usiku baada ya abiria wa awali kuhudumiwa na kuondoka.
“hawa walielekezwa kushuka uwanja wa KIA kutokana na sababu za kiufundi zilizopelekea ndege ya KLM kutokuelekea Dar es Salaam na katika awamu hii abiria hawa 91 walihudumiwa wastani wa dakika mbili kwa kila abiria,ambapo walianza kuhudumiwa mnamo saa 5:50 hadi saa 6:35 usiku,”amesema.
Amesema kuwa, wamefanya uchunguzi na kujiridhisha kuwa aliyefanya kitendo hicho cha kurekodi na kusambaza Video hiyo iliyoleta taharuki nchini na duniani kote ni raia wa Tanzania, ambaye ameonyesha kuwa siyo mzalendo kwa Taifa letu na ana nia ovu ya kufifisha jitihada za Rais Samia katika kukuza utalii nchini kupitia filamu ya Royal Tour.
Mselle alisema kuwa,Idara ya Uhamiaji inapenda kuujulisha umma kuwa kwa mujibu wa viwango vya kimataifa vya Shirika la Usafiri wa Anga duniani-(ICAO) abiria mmoja anastahili kuhudumiwa kwa muda usiozidi dakika tatu,”amesema .
Ameongeza kuwa, taarifa iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii siyo sahihi, kwani abiria wote walihudumiwa kwa mujibu wa taratibu na viwango vya Kimataifa vya kuhudumia abiria katika viwanja vya ndege
Aidha ametoa wito kwa watanzania kuwa wazalendo kwa nchi yao na kusaidia jitihada za kukuza uchumi kupitia sekta ya utalii.