***********************
Na Mwandishi wetu, Babati
SHIRIKA la Civil Social Protection Foundation (CSP) kwenye maadhimisho siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia nchini, wametoa elimu ya kujilinda na ubakaji na ulawiti kwa wanafunzi wa shule ya msingi Darajani Mjini Babati Mkoani Manyara.
Mkoa wa Manyara unaongoza nchini kwa asilimia 58 kwenye matukio ya ukeketaji na unashika nafasi ya pili baada ya Iringa kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kuripotiwa matukio zaidi ya 6,000 kwa mwaka jana.
Mwanasheria wa shirika hilo la CSP Eliakim Paulo amesema wametoa elimu hiyo kwenye shule tatu za msingi Darajani, Oysterbay na Babati.
Paulo amesema matukio ya ukeketaji, ubakaji na ulawiti yanawaathiri watoto hivyo wanatoa elimu hiyo kwa wanafunzi hao ili kuhakikisha matukio hayo yanamalizika.
“Watoto ni kundi maalum hivyo hawawezi kujitegemea au kujilinda wao wenyewe hivyo tunawapa elimu ili wajitambue na kuweza kuepuka hayo,” amesema Paulo.
Amesema wataendelea kutoa elimu ya kupinga matukio ya ukatili wa kijinsia kwenye shule nyingine ili wanafunzi hao wazidi kujitambua na kuepuka kufanyiwa ukatili.
Amesema watatoa elimu hiyo kwa jamii hususani kwa wanawake na watoto katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo ili kuhakikisha matukio ya ukatili wa kijinsia yanakomeshwa.
“Pamoja na shule za msingi pia tutatoa elimu hii kwenye mikusanyiko ya watu ikiwemo hospitalini, minadani na nyumba za ibada,” amesema Paulo.
Ofisa maendeleo ya jamii kutoka halmashauri ya mji wa Babati, Farida Sekiete amewataka watoto hao wasikubali mtu yeyote ashike sehemu zao za siri.
“Usikubali mtu akushike hapa mbele au kwenye makalio na matiti kwa wasichana na endapo ikitokea utoe taarifa kwa mzazi au mwalimu,” amesema Sekiete.