Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt. Mwinyi Talib Haji akipimwa presha na wingi wa damu na Dokta kutoka Hospitali ya Mnazi mmoja Asha Mohammed Ali katika zoezi la upimaji lililofanyika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Mazizini Mjini Zanzibar.
Naibu Mwanasheria Mkuu Zanzibar Ramadhan Abdallah Haji akifurahia majibu aliyopatiwa na Dkt. Bigwa wa sukari kutoka Mnazimoja Faidha Kassim Suleiman baada ya kumaliza vipimo katika zoezi la upimaji afya huko afisini kwao Mazizini Mjini Zanzibar.
Mkurugenzi Idara ya Uwandishi wa Sheria Hassan Ali Haji akifanyiwa vipimo vya Presha na Wingi wadamu na daktari kutoka Mnazi mmoja Asha Mohammed Ali katika zoezi la kupima Afya za wafanyakazi wa ofisi hiyo lililofanyika Afisini kwao Mazizini Mjini Zanzibar.
Mfanyakazi wa Afisi ya Mwanasheria Mkuu ambaye pia ni wakili wa Serikali Zaitun Simba Abdallah akipimwa presha na wingi wa damu na dokta Saada Khalfan Haji katika zoezi la kuchunguza Afya za wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu lililofanyika Afisini kwao Mazizini Mjini Zanzibar.
Wafanyakazi wa Afisi ya mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wakisubiri huduma ya vipimo vya Afya katika zoezi la kupima afya wafanyakazi hao lililofanyika Ofisini kwao Mazizini Mjini Zanzibar.
…………………….
Na Faki Mjaka-Zanzibar
Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dkt. Mwinyi Talib Haji amesema katika kupambana na Magonjwa mbali mbali Ofisi yake imejiwekea utaratibu wa kupima afya za wafanyakazi wote wa ofisi hiyo kila baada ya muda ili kujihakikishia afya njema katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Baada ya zoezi la upimaji wa afya kumalizika Madaktari dhamana hutoa majibu na ushauri wa kitaalaam ili wafanyakazi hao waendelee kufuata miongozo hiyo ambayo itawaweka salama dhidi ya magonjwa.
Akizungumza baada ya kumaliza kufanya vipimo Dk. Mwinyi amesema umekuwa ni utaratibu uliozoeleka kwa ofisi hiyo kujua hali za afya zao kwa ushirikiano mkubwa wanaoupata kutoka kwa Madaktari bingwa wa hospitali ya Mnazi mmoja.
“Kwa kweli huu ni utamaduni wetu hapa, hata watangulizi wangu walikuwa wanafanya zoezi la kupima afya ambalo kimsingi kila mmoja anafahamu umuhimu wa afya njema kwa wafanyakazi katika kukabiliana na majukumu yao” alisema Dk. Mwinyi.
Ametoa wito kwa Taasisi nyingine kupima afya za wafanyakazi wao kwani kwa kufanya hivyo kutahakikisha kuwa na wafanyakazi na jamii yenye afya njema na uwezo wa kutekeleza vyema majukumu.
Kwa upande wake Daktari Bigwa wa Ugonjwa wa sukari kutoka Mnazimoja Faidha Kassim Suleiman amesema zaidi ya wafanyakazi 70 wamefanyiwa vipimo vya magonjwa mbali mbali ikiwemo Sukari, Presha na Uzito na kutoa ushauri wa kitaalam.
Akifafanua zaidi amesema wapo watu wawili waliobainika na Sukari lakini wenyewe wanajifahamu juu ya tatizo hilo na wapo wawili wengine ambao hawakuwa wanafahamu kuwa wana tatizo hilo. Hivyo amewafamisha namna ya kukabiliana na ugonjwa huo ili kuepuka madhara zaidi.
Akigusia kuhusu tatizo la uzito Dk. Faidha amesema takriban Nusu ya wafanyakazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wana uzito mkubwa jambo ambalo ni hatari kiafya.
Amesema tatizo la uzito ni kubwa katika jamii lakini hata katika ofisi hiyo hali si nzuri kutokana na baadhi ya wafanyakazi kuwa na uzito unaoleta mashaka kwa musktakabali wa afya za wafanyakazi hao.
Amesetoa rai kwa wafanyakazi hao kuhakikisha wanafanya juhudi mbali mbali ili kupunguza uzito unaoweza kusababisha magonjwa mengine katika miili yao.
“Hapa kwa Mwanasheria kipo chumba maalum cha kufanya mazoezi GYM. Tumeiona GYM na tumezungumza na Uongozi ili kuwapangia ratiba rasmi wale ambao uzito wao unahatarisha afya zao wapunguze kile” amesema Dk. Faidha.
Awali Naibu Mwanasheria Mkuu Zanzibar Ramadhan Abdallah Haji alisema afya kwa kila binadamu ni muhimu na mtu anapokuwa na afya njema inamrahisishia utendaji kazi wa majukumu ya kila siku.
Amesema kwa kulitambua hilo ndio maana ofisi yao huwajibika kupima afya za wafanyakazi wote kupitia madaktari bingwa na kutoa ushauri na miongozo ya kitaalamu inayosaidia wafanyakazi hao kuchunga afya zao.