Muonekano wa vifaa vilivyopokelewa na Bohari ya Dawa (MSD)
Vifaa hivyo vikiwa kwenye maboksi
Na Mwandishi Wetu
Katika kuadhimisha Siku ya UKIMWI Duniani MSD imeendelea kupokea na kusambaza bidhaa mbalimbali za afya za
kupambana na kudhibiti maambukizi ya Virusi vya UKIMWI.
Mkurugenzi Mkuu wa MSD Mavere Tukai ameeleza kuwa miongoni mwa bidhaa za
afya ambazo kwa sasa inauhitaji mkubwa na inaendelea kusambazwa na MSD kwenye
vituo vya kutolea huduma za afya ni vipimo vya kupima maambukizi ya Virusi vya
UKIMWI na gonjwa la zinaa la Kaswende ( HIV/ Syphilis Duo).
Vipimo hivyo vinafadhiliwa na Mfuko wa Dunia wa kupambana UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (The Global Fund) na pia hutumika kupima
akina mama wajawazito kutambua maambukizi ya magonjwa yote mawili kwa wakati
mmoja.
Kwa mujibu wa Dr. Ibadi Kaondo wa MSD, vipimo hivyo vinamsaidia mama
mjamzito kutambua hali ya afya mapema, na endapo maambukizi yamegundulika
inarahisisha kuanza matibabu mapema ili kufubaza makali ya virusi vya
ukimwi na kutibu kaswende kwa ajili kuimarisha afya ya mzazi na kumkinga mtoto
dhidi ya Maambukizi ya VVU, Kaswende ama kujifungua mtoto mfu.
Hapo
awali vipimo hivi kila kimoja kilikuwa kinajitegemea, ambapo vilitumia muda
mrefu kutoa majibu. MSD kwa sasa ina shehena ya kutosha ya vipimo
hivyo ambavyo tayari baadhi vilishaanza
kusambazwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.