KATIBU Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo) Tixon Nzunda,akizungumza wakati akifungua kikao cha wadau cha maboresho ya kodi na tozo katika sekta ya mifugo kilichofanyika leo Novemba 29,2022 jijini Dodoma.
SEHEMU ya Wadau wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo) Tixon Nzunda, wakati akifungua kikao cha wadau cha maboresho ya kodi na tozo katika sekta ya mifugo kilichofanyika leo Novemba 29,2022 jijini Dodoma.
KATIBU Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo) Tixon Nzunda,akiwa katika picha ya pamoja na wadau mara baada ya kufungua kikao cha wadau cha maboresho ya kodi na tozo katika sekta ya mifugo kilichofanyika leo Novemba 29,2022 jijini Dodoma.
…………………………………..
Na Alex Sonna-DODOMA
KATIBU Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Mifugo) Tixon Nzunda amesema wameenda Mashamaba darasa 100 ya malisho ya mifugo kwa ajili ya wafugaji ili waweze kuzalisha malighafi hiyo ili kuongeza tija.
Hayo ameyasema leo Novemba 29,2022 jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha wadau cha maboresho ya kodi na tozo katika sekta ya mifugo
Bw.Nzunda amesema kuwa lengo la kuandaa mashamba hayo ni kuongeza tija ya uzalisaji wa malisho kwa wafugaji na kuondoa dhana ya utegemezi.
“Tutakuwa na mashamba darasa 100 ambayo ni maalumu kwa ajili ya kuwaonyesha wafugaji wadogo namna ya kufuga na kuwa na malisho ili kuokoa mifugo wakati wa hali mbaya ya ukame , njaa na dharura.”amesema Bw.Nzunda
Aidha amesema kuwa kila mmoja atambue kuwa wameanza kuwekeza ili wafugaji wetu wapate faida na kuondokana na dhana ya kuona serikali ina wajibu wa kufanya kila kitu.
Hata hivyo ameelezea lengo la kuandaa kikao hicho ni kujenga uelewa wa pamoja kwa kupitia maombi ya kufuta tozo na kodi mbalimbali zilizoombwa mwaka huu wa fedha na kujadili maombi mapya.
“Tumekuwa na desturi ya kuomba kodi na tozo mbalimbali zipunguzwe au kufutwa lakini ni vyema tukawa na utamaduni pia wa kuleta mapendekezo ya namna serikali itakavyoweza kupata vyanzo vipya vya mapato kutoka kwenye sekta yetu ya mifugo,”amesema
Amesema kuwa mwaka jana kuliwasilishwa maombi ya kupunguza au kufutiwa kodi na tozo 45 kati ya hizo maombi 42 yalikubaliwa kwa kupunguzwa au kufutwa kabisa.
“Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kupunguza kodi na tozo tulizoziomba mwaka jana na kupelekea kuongeza biashara ya ndani na nje ya nchi kwenye sekta ya mifugo.
Naye Mdau wa sekta ya mifugo ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti Baraza la Kilimo Tanzania (ACT), Jitu Viajlal Son amesema katika kikao hicho watajadili changamoto mbalimbali ambazo wanakumbana nazo na kuziwasilisha kwa katibu Mkuu kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi.