Na Mapuli Misalaba, Shinyanga
Viongozi wa Jukwaa la mtandao wa kijamii la WhatsApp linalojulikana kwa jina la SHY TOWN VIP Mkoa wa Shinyanga wametoa msaada wa Magodoro na Madaftari kwa wanafunzi wa shule ya Buhangija jumuishi wanaoishi bweni.
Vifaa hivyo vilivyo tolewa leo na wanachama wa Shinyanga VIP ni msaada kufuatia maafa yaliyotokea katika shule hiyo ambapo hivi karibuni bweni la wanafunzi wasichana liliteketea kwa moto na kusababisha vifo na kuteketea kwa samani ikiwemo vitanda, magodoro na vifaa vingine vya wanafunzi.
Akikabidhi msaada huo Mwenyekiti wa kikundi cha SHYTOWN VIP Bwana Mussa Ngangala amewataka walimu na wanafunzi wa shule hiyo kuwa watulivu na wenye subira baada ya maafa hayo kujitokeza kwa kuwa serikali na wadau wengine mbalimbali wataendelea kushirikiana nao kutatua changamoto zilizopo.
Ngangala ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri ya CCM Mkoa wa Shinyanga amesema chama cha mapinduzi CCM kitaendelea kusimamia utekelezaji wa ilani ili kuhakikisha upatikanaji wa huduma za kijamii zinapatikana ikiwemo kutimiza mahitaji ya elimu katika shule hiyo.
“Baada ya kupata taarifa juu ya tukio hili tukasema ni vyema sisi sote tuungane kwa pamoja kama Group la SHYTOWN VIP na tulifanya mawasiliano na wewe mkuu wa shule ukatueleza mahitaji yakiwemo Magodoro kama tulivyoweza kutekeleza kwa upande wa watoto msisikitike wala msisononeke na wala msijione mmetengwa au mmebaguliwa niwatie moyo kwamba sisi ndugu zenu tuko pamoja na wala hamko peke yenu”.amesema Ngangala
“Leo hii tumekuja na zawadi hii kwenu kwa ajili ya kufidia pale ambapo pamepotea hatuwezi kuyamaliza mahitaji yote sisi ila kwa umoja wetu tunweza tukapunguza mahitaji niseme pole sana katika kituo hiki lakini serikali yetu ya jamhuri ya muungano wa Tanzania ni kuhakikisha kwamba ipo pamoja na ninye chama cha mapinduzi kinawapenda na yote haya tunayoyaona ni matunda ya chama cha mapinduzi kwa sababu inaisimamia serikali mpaka sasa hivi ni tulivu”.amesema Ngangala
Kwa upande wake Mwalimu mkuu wa shule hiyo Bi.Fatuma Hamis Gilala, amewashukuru kwa msaada huo ambao utasaidia kupunguza mahitaji ya vifaa mbalimbali vinavyohitajika tangu kuungua kwa bweni la wanafunzi wa kike shuleni hapo.
“Tunashukuru sana kikundi cha SHYTOWN VIP kwa namna mlivyoguswa tuka janga hili lilipotokea na hata leo imewapendeza mmeona ni vyema kuja kutupatia neno la faraja kututia moyo lakini pia kuwa sehemu ya kugusa mahitaji tuliyonayo baada ya janga hili kutukuta tumekuwa na mahitaji makubwa ya magodoro lakini leo mmetuletea magodoro kwa ajili ya kuhakikisha usalama katika zoezi zima la kulala kwa kweli tunamuomba sana Mungu awabariki.”amesema mkuu wa shule Fatuma
Wadau mbalimbali wameendelea kushirikiana na serikali kupeleka misaada mbalimbali katika shule ya msingi Buhangija jumuishi iliyopo katika Manispaa ya Shinyanga, baada ya bweni moja kuteketea kwa moto hivi karibuni na kusababisha vifo vya wanafunzi watatu na samani mbalimbali ikiwemo magodoro kuteketea.