Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Mwenyekiti wa Makampuni ya Lodhia Group, Arun Lodhia wakati alipowasili kwenye kiwanda cha nondo na mabomba cha kampuni hiyo kilichopo Mkuranga akiwa katika ziara ya Mkoa wa Pwani,
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akitazama uzalishaji wa nondo wakati alipotembelea kiwanda cha Nondo cha Makampuni ya Lodhia Group kilichopo Mkuranga akiwa katika ziara ya Mkoa wa Pwani, Novemba 28, 2022. Kulia ni Mwenyekiti wa Makampuni hayo Arun Lodhia.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda cha mabati cha Makampuni ya Lodhia Group kilichopo Mkuranga akiwa katika ziara ya Mkoa wa Pwani Novemba 28, 2022. Wa tatu kulia ni Mwenyekiti wa Makapuni hayo Arun Lodhia, kushoo ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange, Wa pili kushoto ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, na Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega na wa tatu kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge. (PIcha na ofisi ya Waziri Mkuu)
.………………………………….
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuwaunga mkono wawekezaji ili kuhakikisha uwekezaji wao haukwami bali unakua na kuleta tija.
Amesema hayo jana (Novemba 28, 2022) alipotembelea na kuweka jiwe la msingi la kiwanda cha kutengeneza mabati cha Lodhia kilichopo Mkuranga Mkoani Pwani.
Mheshimiwa Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali ina dhamira ya dhati ya kuhakikisha wawekezaji nchini wanapata faida “tunathamini uwekezaji huu, tunaheshimu uwekezaji huu na tutakuunga mkono kwenye uwekezaji”
Amesema kuwa Wawekezaji wamekuwa na mchango mkubwa katika kuchangia marndeleo ya nchi katika sekta mbalimbali ikiwemo Afya, elimu, kilimo, mawasiliano na hata ajira “ Upanuzi wa kiwanda hiki ni kumuunga mkono Rais Samia katika jitihada zake za kuendelea kupunguza changamoto ya upatikanaji wa ajira kwa watanzania”
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa uwepo wa wawekezaji ikiwemo katika sekta ya viwanda wanaisaidia nchi kwa kiasi kikubwa kuwa na uhakika wa upatikanaji wa bidhaa ndani ya nchi badala ya kuagiza kutoka nje pekee “Leo hii hatuna haja sana ya kuagiza nondo Ulaya au Asia, nyingi zinapatikana hapa nchini ikiwemo kwenye kiwanda hiki cha Lodhia”
Aidha Waziri Mkuu amewataka wafanyakazi wa kampuni hiyo kuwa mabalozi wazuri kwa kufanya kazi kwa weledi na uaminifu ili kuhakikisha malengo ya muwekezaji yanatimia “Endeleni kufanya kazi vizuri kwenye kampuni hii, ninyi ni mabalozi wetu wazuri”