WAZIRI wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha Wanawake na Vijana wa Bara la Afrika kutumia fursa na kushiriki kikamilifu kwenye biashara katika Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA).
Ameyasema hayo Novemba 25, 2022 wakati akimwakilisha Rais katika Mkutano wa Dharula wa 17 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika kuhusu Maendeleo ya Viwanda Barani Afrika uliofanyika Novemba 20-25, 2022 Jijini Niamey Niger.
Aidha, Wakuu hao wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika wamempongeza Rais kwa kuandaa Kongamano la Kwanza la AfCFTA la Wanawake na Vijana Wafanyabiashara ambalo lilifanyika Jijini Dar es Salaam mwezi Septemba lililohimiza kutoa kipaumbele kwa wanawake na vijana na wakati wa utekelezaji wa mkataba wa AfCFTA ili kuwainua kibiashara na kiuchumi.
Amesema Salamu hizo za pongezi kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kutoka kwa Marais wenzake ni uthibitisho mwingine wa kuendelea kuaminiwa na kukubalika kimataifa kwa uongozi wake mahiri ambao umejipambanua katika kuleta maendeleo jumuishi kwa makundi mbalimbali ya kijamii ikiwemo wanawake na vijana.
Amesema katika agenda ya Maendeleo ya Viwanda Barani Afrika na Uanuai wa Uchumi (Industrialization and Economic Diversification) Wakuu wa Nchi na Serikali hizo wamekubaliana kuweka mikakati ya pamoja katika uendelezaji wa viwanda na uimarishaji wa uchumi wa bara la Afrika kwa kuweka sera na mipango sahihi ya kuwezesha maendeleo ya viwanda barani Afrika.
Aidha, akiwa katika mkutano huo, Waziri Kijaji amesisitiza kuwa Tanzania iko tayali kuendelea kuunga mkono juhudi za uendelezaji wa Viwanda barani Afrika kwa kuongeza thamani malighafi za aina mbalimbali zinazopatikana Afrika ili kupunguza kuagiza bidhaa hizo pamoja na kutengeneza nafasi za ajira kwa wananchi.
Kwa upande wa agenda ya Eneo Huru la Biashara Afrika (African Continental Free Trade Area – AfCFTA) amesema taarifa ilitolewa kuhusu kukamilika kwa majadiliano kwenye Itifaki za Uwekezaji, Sera za Ushindani na Haki Miliki za Ubunifu ambazo sasa zitapitishwa kwenye Mkutano ujao wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa mwezi Februari 2023
Vilevile Waziri Kijaji amewasisitiza watanzania wazalishaji wa bidhaa kujiweka tayari kutumia fursa ya soko la AfCFTA kwa Tanzania ni miongoni mwa nchi saba ambazo zitaanza kuuza bidhaa zake kwa kutumia kanuni za AfCFTA kuanzia mwezi Juni 2023. Nchi nyingine ni Cameroon, Kenya, Misri, Ghana, Mauritius, Rwanda.