Mkataba wa upanuzi wa mfumo wa majita ukisainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele (kushoto) na Katibu Mtendaji wa LVBC, Dkt. Masinde Bwire (kulia),wanaoshuhudia ni viongozi wa Wizara ya Maji na MWAUWASA.
Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA, Mhandisi Leonard Msenyele (kushoto) na Katibu Mtendaji wa LVBC, Dkt.Masinde Bwire wakibadilishana hati za mkataba mara baada ya kusaini.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira, Mhandisi Charles Mafie (kushoto) akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga ,wakati wa hafla ya kutia saini mkataba wa upanuzi wa mfumo wa majitaka
Wawakilishi wa LVBC, Wizara ya Maji, Bodi na Menejimenti ya MWAUWASA mara baada ya kushuhudia utiaji saini wa mkataba wa upanuzi wa mfumo wa majitaka.Picha zote na Baltazar Mashaka
*********************
NA BALTAZAR MASHAKA,MWANZA
MAMLAKA ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) kwa niaba ya serikali imesaini mkataba wa sh.bilioni 12.7 na Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) kwa ajili ya upanuzi wa mfumo wa majitaka utakaonufaisha wakazi 7,360 jijini Mwanza.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Maji,Mhandisi Anthony Sanga,Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira,Mhandisi Charles Mafie katika utiaji saini wa mkataba huo juzi alipongeza jitihada za LVBC kutunza Ziwa Victoria.
Alisema wananchi wanahitaji maji safi na salama, hivyo jitihada za makusudi za kutunza vyanzo vya maji zisipofanyika,maji salama hayatapatikana.
“Mwanza kwa mkataba huu na programu hii tunakwenda kuhakikisha Ziwa Victoria linalindwa na sio suala la maji pekee,ziwa likichafuka maana yake hata samaki hatutapata.Pia hapa tunazungumzia suala la lishe,” alisema Mhandisi Mafie.
Aliishauri LVBC kutazama jinsi ya kutanua mpango huo na kuufikisha kwenye miji mingine inayozunguka Ziwa Victoria ikiwemo miji ya Musoma na Bukoba ili kusiwe na uchafuzi kwenye maeneo yote yanayolizunguka ziwa hilo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa MWAUWASA,Mhandisi Leonard Msenyele alisema mradi huo utanufaisha wakazi 7,360 wa Kata za Igogo,Kitangiri,Kirumba,Pasiansi na Nyamanoro .
Alieleza kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha maji ya Ziwa Victoria yanaendelea kuwa salama kutokana na jitihada,mikakati na hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na uwepo wa mradi huo.
“Tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan,kutuletea mradi huu,sisi kama taasisi tutanufaika kwani kulinda uchafuzi wa ziwa itasaidia kupunguza gharama ya kutibu maji kabla ya kuyapeleka kwa wananchi,” alisema Mhandisi Msenyele.
Mkurugenzi Mtendaji huyo wa MWAUWASA aliihakikishia serikali kuwa itasimamia utekelezaji wa mradi kwa eweldi kulingana na thamani ya fedha na kila kipengele kwenye mkataba kitasimamiwa kwa kuzingatia miiko ya kitaaluma ili kuleta tija kwa jamii.
“Serikali kupitia Wizara ya Maji, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Wizara ya Fedha na Mipango imetuamini kusimamia mradi huu,hivyo tunaahidi kuutekeleza kwa uaminifu mkubwa ili manufaa yaliyokusudiwa yapatikane,” alisema Mhandisi Msenyele.
Naye Katibu Mtendaji,Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC), Dkt.Masinde Bwire alisema chimbuko la mradi huo linatokana na mradi wa kwanza wa Uhifadhi wa Mazingira ya Ziwa Victoria (LVEMP) ambao haukutatua changamoto zote kwa wakati huo ikiwemo ya uchafuzi wa ziwa.
“Mradi huu umeainisha changamoto zilizoshindwa kutatuliwa na mradi wa LVEMP, hadi sasa uchafuzi wa Ziwa Victoria bado ni mkubwa kutoka kwenye miji inayolizunguka ikiwemo Mwanza, Kampala, Kisumu, Musoma na Bukoba,” alisema.
Dkt.Bwire alieleza kuwa jukumu kubwa la LVBC ni kusimamia matumizi endelevu ya Rasilimali za Maji na zingine ndani ya ukanda wa Ziwa Victoria na ni wajibu wao kutafuta fedha kwa kushirikiana na Serikali za Jumuia sambamba na wadau wa mazingira na maendeleo.
“Tumepata sh. bilioni 12.7 za Kitanzania kwa ajili ya mradi huu unaotekelezwa kupitia Mpango Jumuishi wa Usimamizi wa Rasilimali za Maji katika Bonde la Ziwa Victoria (‘LVB IWRMP’) na utasimamiwa na MWAUWASA,” alisema.
Katibu Mtendaji huyo wa LVBC alisema utakamilika mwishoni mwa mwaka 2025 na jitihada za kutafuta fedha zaidi kutoka kwa wadau zinaendelea kwa sababu uchafuzi wa Ziwa Victoria bado ni mkubwa.
“Rai yetu kwa Mamlaka za Miji inayozunguka Ziwa Victoria ni kuendelea kuhimiza usafi wa mazingira na kufanya matumizi endelevu ya Rasilimali za Maji na vyanzo vya maji,”alisistiza Dkt. Bwire.