Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Mhandisi Clement Kivegalo katikati akiangalia mchoro wa mradi wa maji unaojengwa kupitia fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uvico-19,mradi huo unatarajiwa kumaliza tatizo la maji katika mji wa Ludewa,kulia meneja wa mamlaka ya maji Ludewa Enock Ngoyinde.
Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Mhandisi Clement Kivegalo kulia,akimtwisha ndoo ya maji mkazi wa mji wa Ludewa mkoani Njombe Veni Lingalangala.
Moja kati ya tenki la maji lenye uwezo wa kuchukua lita 5,000 lililojengwa kupitia fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya Uvico-19 ambalo litahudumia wakazi wa Mji wa Ludewa.
**************************
Na Muhidin Amri,
Ludewa
SERIKALI imetoa zaidi ya Sh.bilioni 7 kwa wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa),kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa maji katika mji wa Ludewa mkoani Njombe.
Mkurugenzi Mkuu wa Ruwasa Mhandisi Clement Kivegalo alisema hayo jana, wakati akizungumza na baadhi ya wananchi na viongozi wa wilaya ya Ludewa akiwa katika ziara yake ya kukagua na kutembelea miradi ya maji mkoani Njombe.
Alisema,kwa sasa Serikali kupitia Ruwasa iko katika mchakato wa kumpata mkandarasi atakayeweza kutekeleza mradi huo unatarajiwa kumaliza kabisa tatizo la maji kwa wananchi wa Mji wa Ludewa na vijiji vya jirani kwa asilimia mia moja.
Amewaagiza viongozi wa Ruwasa wilaya ya Ludewa na mkoa wa Njombe,kuhakikisha wanatafuta mkandarasi mwenye uwezo mkubwa wa kifedha ambaye atatekeleza kazi kwa wakati na bila usumbufu wowote.
“Kwanza naagiza wataalam wangu wamtafute mkandarasi mwenye nguvu ya kifedha ambaye akianza kutekeleza kazi ya Sh. milioni hamsini kati ya bilioni 7 asisimame,tunamtaka mkandarasi ambaye hata fedha zikichelewa aendelee na kazi ili wananchi wafaidi matunda ya serikali yao”alisema Kivegalo.
Aidha,amewataka wataalam wa Ruwasa kushirikiana na wadau wengine wa sekta ya maji wakiwamo wataalam wa mabonde ya maji,kuhakikisha wanadhibiti na kutunza vyanzo vyote vya maji ili mradi huo uliosanifiwa kufanya kazi kwa miaka ishirini ijayo uwe endelevu kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Kivegalo ameishukuru Serikali kutoa fedha hizo na kuhaidi kuwa,zitafanya kazi kama ilivyokusudiwa na kuwahakikishia wananchi wa Ludewa kuwa, huduma ya maji katika mji huo itakuwa safi na salama.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji katika mji mdogo wa Ludewa Enock Ngoyinde alisema,mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya Sh.bilioni 7.4 na utahudumia zaidi ya wakazi 15,661 ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia ishirini na tatu.
Mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamoga,ameipongeza serikali ya awamu ya sita kuendelea kuipatia wilaya ya Ludewa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika vijiji mbalimbali vya jimbo la Ludewa.
Alisema, katika kipindi kifupi serikali kupitia wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa), imefanikiwa kutekeleza miradi ambayo imewezesha kupunguza kama sio kumaliza kabisa changamoto ya maji safi na salama kwa wakazi wa jimbo hilo.
Hata hivyo,ameiomba wizara ya maji kujenga miradi mingine katika vijiji vilivyopo kando kando ya Mto Ruhuhu ili kuwanusuru wananchi na hatari ya kuliwa na wanyama wakali hasa mamba na kutumia maji ya mto huo ambayo hayafai kwa matumizi ya binadamu kutokana na shughuli za uchimbaji wa madini.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Ludewa Monica Mchilo alisema,wananchi wa Ludewa wana changamoto kubwa ya maji safi na salama na kusababisha baadhi ya shughuli za maendeleo kusua sua kwani wananchi wanatumia muda mwingi kwenda kutafuta maji ambayo yanapatikana mbali na makazi yao.
MWISHO.