Na Dotto Mwaibale, Singida
WANANCHI wa Kata ya Ntuntu Walayani Ikungi mkoani hapa wanatarajia kuanza kupata huduma za kitabibu katika Kituo kipya Cha Afya Cha Ntuntu baada ya ujenzi wake kukamilika kwa asilimia 99.
Akizungumza hivi karibuni wakati wa ziara yake Mkurugenzi wa Huduma za Afya Lishe na Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR- TAMISEMI) Dkt.Ntuli Kapologwe amesema ifikapo jumatatu ya Novemba 28 mwaka huu kituo hicho kiwe kimeanza kazi na kuhudumia wananchi.
Aidha ameeleza kwamba hatua iliyofikia kituo hicho inastahili kuendelea kutoa huduma kwa wananchi wa maeneo hayo wakati vitu vidogo vidogo vilivyobaki vikiendelea kukamilishwa.
Hata Hivyo Dkt.Kapologwe ameagiza Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kwa kushirikiana na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida kuendelea na maandalizi ya kupokea vifaa tiba ili ifikapoa Novemba 28,2022 huduma ziwe zimeanza na wananchi wanapata matibabu.
“Tumeambiwa jengo limefikia asilimia 99 kukamilika kwa hatua hii ni lazima huduma zianze kutolewa hata kama kuna vitu vichache vya kumalizia ” alisema.
Hata hivyo ameendelea kueleza kwamba Serikali ipo hatua ya mwisho ya kuleta vifaa tiba katika kituo hicho ambapo amesema kufikia jumatatu vitakuwa vimeshafika.
“Serikali ipo kwenye hatua za mwisho za uletaji wa vifaa tiba mbalimbali katika kituo cha afya hivyo wananchi waanze kupata huduma” alisema Dkt. Kapologwe.
Dkt. Kapologwe ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi na timu nzima ya usimamizi wa ujenzi wa kituo hicho cha afya kwa ukamilishaji mzuri wa majengo matatu ya awamu ya kwanza (Jengo la Wagonjwa wa Nje OPD, Jengo la Maabara na Kichomea Taka) ambao mpaka sasa umekamilika kwa asilimia 99% .
Aidha majengo matatu mengine ni pamoja na Jengo la Wodi ya Wazazi (Maternity), Jengo la Upasuaji (Theatre) na Jengo la Kufulia (Laundry) ambapo ujenzi huyo umefikia zaidi ya asilimia 60% huku Dkt.Kapolongwe akiwataka kuongeza kasi ya ujenzi ili kufikia Disemba 30 majengo hayo yawe yamekamilika.
Ujenzi wa vituo vya afya ni moja ya mkakati na kipaumbele cha serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya katika maeneo ya karibu na makazi yako.