Mkuu wa kitengo cha sayansi asilia kutoka UNESCO ,Kelvin Robert akizungumza na waandishi wa habari juu ya mkutano huo,katikati ni Kamishna msaidizi mwandamizi wa uhifadhi kutoka NCAA ,Mhandisi Joshua Mwankonda ,na aliyeko kulia ni Mkuu wa kitengo cha mawasiliano NCAA,Joyce Mgaya
…………………..
Julieth Laizer ,Arusha.
Arusha.TANZANIA inatarajiwa kuwa mwenyeji wa mkutano wa wataalamu wa Tafiti za Hifadhi ya Asili na Tamaduni kutoka katika Nchi 52 Duniani katika kuadhimisha miaka 50 ya Mkataba wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya Elimu ,Sayansi na Utamaduni( UNESCO) utakaofanyika desemba 12 hadi 14,2022.jijini Arusha.
Hayo yamesemwa jijini Arusha na Mkuu wa kitengo cha sayansi asilia kutoka UNESCO Kelvin Robert wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema Tanzania kuwa mwenyeji wa Maadhimisho hayo ni kutokana na kukidhi vigezo vyote vilivyoweka na Umoja wa mataifa katika makubaliano ya utekelezaji wake.
Mkutano huo unaandaliwa na UNESCO kwa kushirikiana Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro(NCAA) wenye mlengo wa kujadili utekelezaji wa mkataba huo katika masuala ya urithi wa asili na utamaduni kwa kuwaleta pamoja wataalamu mbalimbali kutoka nchi 52 duniani.
“Pia kigezo kingine cha Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huu ni kutokana na kuridhia mkataba huu nakuanza kuutekeleza tangu mwaka 1977 pasipokuwa na migogoro ya aina yoyote,”amesema Robert.
Robert amesema Tanzania kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo ni fursa katika kuleta nchi za kiafrika kufika nchini kujifunza namna njema walivyotekeleza mkataba huo pamoja na kubadilishana changamoto zinazoikabili ikiwemo wataalamu wa kutosha.
“Ni fursa nzuri kwa Tanzania kuweza kuielimisha dunia na wadau mbalimbali kuhusu mbinu na mikakati iliyoweza kutumika hifadhi ya Ngorongoro inavyosimamiwa kikamilifu kwa kutekeleza mkataba wa mwaka 1972 katika nyanja ya mawasiliano,uwajibikaji,uhifadhi,kujenga uwezo na ushiriki wa jamii,”amesema.
Naye Kamishna Msaidizi mwandamizi Mhadhiri Joshua Mwankonda amesema nchi ya Tanzania imekuwa ikinufaika na mkataba wa urithi wa asili na kiutamaduni katika kujitangaza hali inayosaidia kuongeza watalii katika hifadhi ya ngorongoro hivyo matarajio yao ni kuongeza ubora wa kiwango cha uhifadhi.