![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2022/11/IMG_20221124_140200_754-scaled.jpg)
![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2022/11/IMG_20221124_135314_217-scaled.jpg)
*********************
Na Mwandishi wetu, Babati
MWENYEKITI wa CCM Mkoa wa Manyara, Peter Toima amesema katika kipindi cha uongozi wake hakutakuwa na mtindo wa kukata majina ovyo ya wagombea kwa kuwaonea pindi ukifika wakati wa uchaguzi.
Toima ameyasema hayo wakati akipokelewa nyumbani kwake Kata ya Emboreet Wilayani Simanjiro tangu achaguliwe kushika nafasi hiyo hivi karibuni.
Amesema kwenye kipindi chake cha Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara, atahakikisha wanachama wanaongozwa kwa kufuata haki.
“Hatutamuonea mtu, hatutakata ovyo majina ya watu kwa kuwaonea ila tutaongoza kwa haki na kuwapa ushirikiano wanachama wetu,” amesema Toima.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro Kiria Laizer amesema kwenye mkoa huo kuna simba wa Manyara mmoja tuu Toima, hivyo waliokuwa wanajiita simba wa Manyara wanapaswa kufyata mkia.
Mjumbe wa mkutano mkuu wa CCM Taifa kupitia wilaya ya Simanjiro, Lenganasa Soipey amesema wajumbe wa wilaya za Simanjiro na Kiteto wasingeweza kumpitisha Toima wenyewe ila wakasaidiana na wilaya nyingine.
Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Simanjiro Anna Shinini amesema wajumbe waliamua kugawa viongozi ili Mwenyekiti atoke wilaya ya Simanjiro na MNEC wilaya ya Babati.
Diwani wa kata ya Terrat, Jackson Ole Materi amesema wana CCM wanapaswa kumuunga mkono Toima kwa lengo la kufanikisha CCM ya uchumi.
Diwani wa kata ya Ngorika, Albert Msole amesema kupitia Toima siasa ambazo hazina msingi hazitakuwepo tena kwenye eneo hilo.
Diwani wa Emboreet, Yohana Shinini amesema baada ya Toima kuchaguliwa hivi sasa makundi yamekwisha hivyo aungwe mkono ili awaongoze wanachama.
Diwani wa kata ya Loiborsiret, Ezekiel Lesenga Mardad amesema chama siyo cha mtu mmoja hivyo Toima ni mtu sahihi atakayeivusha Manyara.
Mwenyekiti wa kijiji cha Komolo, Saning’o Sommy amesema maeneo ya chama ya kiuchumi yanapaswa kubainishwa ikiwemo viwanja na mashamba ili kazi ianze ikiwemo ujenzi wa ofisi za matawi na kata.