Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na Gavana, Prof. Florens Luoga, alipotembelea banda la BoT katika Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha yanayofanyika katika Viwanja vya Rockcity Mall jijini Mwanza.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, akipewa maelezo na Gavana, Prof. Florens Luoga alipotembelea banda la BoT katika Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha yanayoendelea katika Viwanja vya Rockcity Mall jijini Mwanza. Kutoka kulia ni Meneja Idara ya Mawasiliano BoT, Bi. Victoria Msina na Naibu Gavana, Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Bi. Sauda Msemo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, akipokea zawadi kutoka kwa Gavana, Prof. Florens Luoga baada ya mazungumzo katika alipotembelea banda la BoT katika Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha yanayoendelea katika Viwanja vya Rockcity Mall jijini Mwanza.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, akisalimiana na Gavana, Prof. Florens Luoga alipofika katika Viwanja vya Rock City Mall Mwanza kufungua rasmi Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, akisalimiana na Naibu Gavana, Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Bi. Sauda Msemo, alipofika katika Viwanja vya Rock City Mall Mwanza kufungua rasmi Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha.
…………………………
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, ameitaka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuhakikisha kuwa huduma za fedha zinafika na kutumika vijijini na kwamba maslahi ya watumiaji wa huduma hizo yanalindwa.
Dkt. Mpango ametoa maagizo hayo alipotembelea banda la BoT katika Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha yanayofanyika katika Viwanja vya Rock City Mall jijini Mwanza ambapo alipokelewa na Gavana wa BoT, Prof. Florens Luoga.
“Mtu anakwenda benki kukopa lakini baadae msaada aliopewa kwenye benki wa kusimamia mradi husika unakosa umakini halafu wanapeleka wanasheria kuuza mali na wanunuzi wa hizo mali wanatoka kwenye benki hizohizo za biashara,”alisema.
Pia, Dkt. Mpango ameitaka BoT kuendelea kufanya kazi kwa karibu na Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA) ili kupunguza viwango vya riba wanavyotozwa wananchi wanapochukua mikopo.
“Najua Benki Kuu imechukua jitihada za makusudi. Ninyi mnakopesha (mabenki) kwa asilimia tatu, lakini wao wanakopesha kwa asilimia tisa. Mfanye kazi kwa karibu na mabenki na TBA mtafute dawa ya riba kuwa juu,” alisema.
Aliongeza kuwa uwepo ya mifumo ya taarifa za wakopaji unatakiwa kuondoa wasiwasi kwa mabenki kutoa mikopo kwa wananchi kwa riba ndogo. “Kama Makamu wa Rais hawezi kukopa basi mjue kuna tatizo kubwa, mimi mwenyewe nasita kukopa na hii sio dalili njema, ” alisema Dkt. Mpango.
Dkt. Mpango ameipongeza Benki Kuu kwa usimamizi madhubuti wa uchumi na sekta ya fedha nchini na kusema kuwa wananchi wana imani na Benki Kuu kama msimamizi wa sekta ya kibenki na hivyo iendelee kuimarisha sekta hiyo kwa maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Awali, Gavana wa BoT, Prof. Luoga, alimweleza Makamu wa Rais kwamba katika kuwalinda watumiaji wa huduma za fedha, Benki zote nchini zimeshiriki kutengeneza kanuni za maadili ambazo zitatumika pia kuwaongeza wafanyakazi wa benki hizo.
“Tumetoa kanuni za kumlinda mtumiaji wa huduma za fedha na kwa sasa Benki Kuu inapokea malalamiko mengi sana na tunayatatua kwa haraka; na pia, tumeanzisha kitengo maalum kinachohusika na kuwalinda watumiaji wa huduma za fedha,” alisema.
Aidha, Gavana Luoga alisema kuwa huduma ndogo za fedha chini ya usimamizi wa Benki Kuu zimeendelea kukua na ni moja ya vipaumbele katika kuimarisha uchumi wetu. “SACCOS zaidi ya 800 na VIKOBA zaidi ya 32,000 tayari vimesajiliwa na tunaendelea kuvisajili ili tuweze kuimarisha sekta ya huduma ndogo za fedha nchini,’’alisema Gavana.
Gavana Luoga alisema, Benki Kuu inaendelea kuimarisha mifumo jumuishi itayowezesha huduma za fedha ziwafikie wananchi kwa gharama nafuu, hiyo ni pamoja na kanzidata ya watoa huduma za fedha nchini ambayo inaiwezesha Benki Kuu kujua watoa huduma hao wanapatikani wapi na aina ya huduma wanazotoa na maeneo yasiyo na huduma za fedha.
“Tunachukua hatua mbalimbali kuwezesha huduma jumuishi za fedha kupatikana kiurahisi na kwa gharama nafuu ili kuhakikisha wananchi wanaweza, sio tu kufikia huduma hizo, lakini pia kuzitumia kuendesha maisha yao ya kila siku,” alisema.
Prof. Luoga aliongeza kuwa Benki Kuu imekamilisha hatua zote za kuanza ujenzi wa hifadhi ya dhahabu ya nchi ambayo itanunuliwa kutoka kwa wachimbaji wadogo wadogo na Benki Kuu itahakikisha dhahabu hiyo inafika na kuhifadhiwa kwa usalama.
Benki Kuu ya Tanzania inashiriki Maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha jijini Mwanza kwa ajili ya kutoa elimu ya fedha kwa umma pamoja na kuwafahamisha wananchi kuhusu majukumu mbalimbali ya Benki Kuu.