Tenki la lenye uwezo wa kuhifadhi lita 200,000 za maji likiwa limekamilika kwa ajili ya kuhudumia wakazi wa kijiji cha Mbangamao wilaya ya Mbinga.
………………………………..
Na Muhidin Amri,
Mbinga
MKURUGENZI wa wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini(Ruwasa) Mhandisi Clement Kivegilo, amewataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya maji katika maeneo mbalimbali mkoani Ruvuma,kuhakikisha wanakamilisha kazi walizopewa kwa mujibu wa makubaliano ya mikataba yao.
Mhandisi Kivegilo ametoa agizo hilo jana,baada ya kutembea mradi wa maji Mbangamao Halmashauri ya Mji Mbinga unaotekelezwa na Ruwasa na kujengwa na Mkandarasi kampuni ya M/S Nipo Africa Engineering kwa gharama ya Sh.bilioni 1,810,439,.89.
Kivegilo,amemtaka mkandarasi huyo kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo ili ukamilike kwa wakati kulingana kwa kuwa wananchi wa kijiji cha Mbangamao wana hamu kubwa ya kupata huduma ya maji ya Bomba.
Alisema,mradi wa maji Mbangamao unatakiwa kumaliza changamoto ya huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa kijiji hicho na maeneo ya jirani,hivyo ni lazima ukamilike haraka ili kuwaondolea wananchi kero ya kutembea umbali mrefu kwenda kutafuta maji kwa ajili ya matumizi yao ya kila siku.
Alisema,kwenye ujenzi wa mradi wa maji ya mserereko hakuna changamoto kubwa katika utekelezaji wake kwa kuwa hata ujenzi wake unaanzia kwenye chanzo tofauti na miradi mingine.
Amemuagiza mkandarasi kuanza ujenzi wa vituo vya kuchotea maji ili wananchi waanze kuwa na matumaini na kuacha visingizio visivyokuwa na sababu kwani tayari ameshapewa sehemu ya fedha kwa ajili ya kazi hiyo na uko nyuma kwa miezi mitatu.
Aidha amemuagiza meneja wa Ruwasa wilaya ya Mbinga Mhandisi Mashaka Sinkara,kushirikiana na viongozi wa serikali ya kijiji hicho ili kupanga bei ya maji ambayo itakuwa rafiki kwa kila mwananchi.
Naye Meneja wa wakala wa usambazaji maji safi na usafi wa mazingira(Ruwasa)wilayani Mbinga Mashaka Sinkara alisema,zaidi ya wakazi 2,900 wa kijiji cha Mbangamao wanatarajiwa kunufaika na mradi huo.
Sinkara alisema,mradi wa maji Mbangamao ni miongoni mwa miradi 8 katika wilaya ya Mbinga inayotekelezwa kwa mfuko wa maji na Serikali kuu,ambapo miradi 7 kati ya hiyo iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji wake.
Kwa mujibu wa Sinkara, kwa sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 60 na unategemewa kukamilika mwezi Januari mwakani baada ya kuongezwa muda wa utekelezaji wake kutoka miezi sita ya awali hadi tisa kutokana na hali ya mvua na upatikanaji wa fedha za awali.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji cha Mbangamao Kasius Sangana,amewaomba viongozi wa Ruwasa kumfuatilia kwa karibu mkandarasi ili aweze kumaliza kazi ya ujenzi wa mradi huo haraka kwa kuwa wananchi wamechoka kusubiri.
Alisema, katika kijiji hicho chenye vitongoji sita kuna changamoto kubwa ya maji ambapo kwa sasa wanalazimika kutembea umbali wa km 6 kwenda kutafuta maji.
Hata hivyo,ameishukuru serikali ya awamu ya sita kupitia wakala wa maji safi na usafi wa mazingira vijijini Ruwasa kwa kuanza ujenzi wa mradi huo ambao unakwenda kumaliza kabisa tatizo hilo la maji.