Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Sara Msafiri wa kushoto akizungumza Jambo na waandishi wa habari hawapo pichani kuhusiana na wiki ya mlipa kodi kulia kwake ni meneja wa TRA Mkoa wa Pwani Emmanuel Maro.
…………………………
Na Victor Masangu,Pwani
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Sara Msafiri ameipongeza Mamlaka ya mapato (TRA) Mkoa wa Pwani kwa kuitumia vizuri wiki la mlipa kodi kwa kuamua kwenda kuwafuata wafanyabiashara mbali mbali katika maeneo yao ya kibiashara kwa kutoa elimu kusikiliza changamoto ili kuweza kuzitafutia ufumbuzi sambamba na kutoa shukrani zao.
Mkuu huyo ameyasema hayo wakati wa kuwatembelea baadhi ya wafanyabiashara wadogo wa kati na wale wakubwa ikiwa ni katika kuadhimisha wiki ya mlipa kodi ambayo imekwenda sambamba na utoaji wa elimu kwa walengwa.
Alisema kwamba TRA wameona kuna umuhimu mkubwa wa kutumia wiki ya mlipa kodi kwa ajili ya kuwafuata wafanyabiashara katika maeneo yao na kuwapa elimu na maelekezo mbali mbali ambayo yataweza kuwasaidia katika utekelezaji mzuri wa kulipa kodi bila vikwazi.
“Mimi kwa kweli nawapongeza TRA kwa uamuzi huu mzuri wa kutoka maofisini na kuamua kuchukua jukumu la kwenda katika maduka mbali mbali pamoja na baadhi ya maeneo ya viwanda hii ni nzuri katika jitihada za kuongeza ukusanyaji wa mapato kupitia elimu ambayo mmewapatia hongereni Sana,”Alisema Sara.
Pia alifafanua kuwa lengo kubwa la serikali ni kuwaletea wananchi wake maendeleo katika huduma mbali mbali za kijamii ikiwemo sekta elimu,afya,maji pamoja na huduma nyingine hivyo wafanyabiashara wanapaswa kutimiza wajibu wao katika kulipa kodi bila kukwepa.
“Kitu kikubwa ninachowaomba ni kuwapa ushirikiano wa kutosha TRA na pindi wanapokuja msiwakimbie kwani lengo ni kujenga kwa pamoja hivyo mnapaswa kutoa ushirikiano kwa kuwa kodi inapokusanywa ndio wananchi wanapata maendeleo kupitia hizi kodi kwa hivyo ni muhimu kweli,”alisema
Kwa upande wake Meneja wa TRA Mkoa wa Pwani Emmanuel Maro alisema kwamba mikakati yao ni kuendelea kushirikiana kwa pamoja na wafanyabiashara ikiwa sambamba na kuwatembelea mara mara ili kuwapa elimu juu ya umuhimu wa kulipa kodi.
Kadhalika alibainisha kuwa lengo lao ni kuweka mazingira rafika ya ulipaji wa kodi katika maeneo yote ya Mkoa wa Pwani ambayo yataweza kuwasaidia wafanyabiashara hao kuendesha shughuli zao bila usumbufu wowote.
Nao baadhi wa wafanyabiashara wa mkoani Pwani wameipongeza TRA kwa kuitumia wiki ya mlipa kodi kwenda kuwatembelea na kuwapa elimu na kuomba jambo hilo liendelezwe kila wakati ili wajifunze mambo mbali mbali.