Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Mohamed Janabi akizungumza na watumishi wa Kijiji cha Marekebisho ya Afya ya Akili Vikuruti
Mkurugenzi wa Tiba MNH Dkt John Rwegasha akizungumza wakati wa ziara ya Prof. Janabi katika Kijiji cha Vikuruti
Baadhi ya watumishi wa Muhimbili Upanga na Vikuruti wakifuatilia
………………………………….
Hospitali ya Taifa Muhimbili ina mpango wa kuanzisha Kliniki ya Magonjwa ya Afya ya Akili ikiwemo huduma jumuishi za waraibu wa dawa za kulevya katika Kijiji cha Marekebisho ya Afya ya Akili, kilichopo Vikuruti Kata ya Chamazi ili kupunguza msongamano uliopo MNH-Upanga.
Tiba Jumuishi (Medical Assisted Treatment-MAT) hutolewa kwa waathirika wa dawa za kulevya ikihusisha ushauri nasaha, matibabu ya kurekebisha tabia pamoja na utoaji dawa aina ya Methadone, ambapo katika Kliniki iliyopo MNH Upanga jumla wa wananchi 1,100 wenye uhitaji huo wanahudumiwa kwa siku.
Mipango hiyo imeelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Mohamed Janabi alipofanya ziara kijijini hapo ambapo alipokea taarifa ya kijiji hicho na kuzungumza na wagonjwa na watumishi.
Aidha Prof. Janabi aliridhishwa na namna kazi za uzalishaji zinavyofanyika kijijini hapo licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali ikiwemo uchakavu wa miundombinu.
“Tutashirikiana na sekta binafsi kuhakikisha tunafanya maboresho makubwa hapa ikiwemo kuzungushia uzio kwenye eneo lote na ekari 160, kujenga majengo mazuri, pamoja na kuanzisha makazi ya kisasa ya kusaidia waraibu wa dawa za kulevya (sober house) ambao watasaidiwa kitaalamu zaidi” amesema Prof. Janabi
Awali akiwasilisha taarifa kwa Mkurugenzi Mtendaji, Mkuu wa Kijiji cha Vikuruti Bw. Beno Kalunga alisema kuwa kwa sasa kijiji kinahudumia wagonjwa 7-10 kwa mwezi, na pia kinajihusisha na kilimo na ufugaji ikiwa ni sehemu ya tiba kazi kwa wagonjwa.
Amesema wagonjwa wanaohudumiwa Vikuruti ni wale waliopata changamoto za afya ya akili na kutibiwa hivyo hupelekwa kijijini hapo kwa lengo la kuendelea na tiba kazi ili afya zao ziimarike vizuri.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Tiba MNH-Upanga, Dkt. John Rwegasha ambaye kitengo hicho kipo chini ya kurugenzi yake alisema kuwa atahakikisha anasimamia utekelezaji wa mipango ya kuboresha kijiji hicho hatua kwa hatua.