*********************
Na. Catherine Sungura, WAF- Dodoma
Watumishi wa Wizara ya Afya wanao wajibu wa kuwezesha jukumu kuu la kuhakikisha na kuwezesha wananchi wanapata huduma bora za afya kote nchini kwa kuhakikisha kila mmoja katika nafasi yake anafanya jukumu lake kwa ufanisi.
Hayo yamesemwa leo na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Bw. Edward Mbanga wakati wa kufungua mafunzo ya huduma kwa mteja (Customer Care) kwa watumishi wa Wizara ya Afya Makao Makuu yanayoendelea kufanyika Jijini Dodoma.
Bw. Mbanga amesema kuwa wananchi wote wanaofika kwenye ofisi za wizara wanatakiwa kupata huduma zinazostahili na kwa wakati bila kukwamisha mfumo wa ufanyaji kazi wa kuwahudumia wananchi.
“Yapo mambo madogo madogo ambayo yanatufanya tuonekane hatuna huduma nzuri kwa wateja, tunapaswa kuwahudumia wananchi wanaofika kwenye ofisi zetu kwani tumeajiriwa kwa ajili ya wateja hao.” Amesema Bw. Mbanga
Aidha, amewataka watumishi hao kufanya kazi bila kinyongo ama kuwakasirikia wananchi wanaofika kwenye dawati lao kanakwamba wapo kwenye biashara zao binafsi na kuonesha wapo hapo kuwahudumia wao wateja wanaokuja.
Ameongeza kuwa itakapofika utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, idadi ya watu wanaoenda kutafuta huduma za afya zitaongezeka kwa sababu kutakuwa na uhakika wa matibabu hivyo inahitaji mkakati mkubwa wa kuboresha huduma kwa mteja katika utoaji wa huduma za afya kote nchini.
“Jiulize wakati ulipoaga unayemuacha nyumbani asubuhi kwamba unaenda kazini hivyo tuwaheshimu wanaokuja katika maeneo tunayofanyia kazi ili tudhihirishe kweli tupo kazini”. Alisisitiza Bw. Mbanga
Pia, Bw. Mbanga aliwataka watumishi hao kutekeleza kwa vitendo yale yote watakayoyapata kupitia mafunzo hayo na hivyo kuwa na dhamira ya kuboresha namna wanavyowahudumia wateja wao.
Naye, Mkurugenzi wa Utawala na Rasiliamali Watu, Wizara ya Afya Bi. Deodhata Makani amesema mafunzo hayo ni muhimu kwa watumishi hao na kuwataka kuzingatia utoaji wa huduma bora kwa wateja wanaofika wizarani na kuongeza kuwa mafunzo hayo yameanza kwa watumishi wa makao mkauu na yatashuka hadi kwa watumishi wengine wa wizara hiyo.