MTENDAJI Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) Dkt.Siston Mgullah,akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Wakala huo na Mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha wa 2022-2023 leo Novemba 15,2022 Jijini Dodoma.
MSEMAJI Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari -MAELEZO Bw.Gerson Msigwa,akizungumza mara baada ya Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM,) Dkt.Siston Mgullah,kutoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Wakala huo na Mwelekeo wa utekelezaji kwa Mwaka wa Fedha wa 2022-2023 leo Novemba 15,2022 jijini Dodoma.
………………………………
Na Alex Sonna-DODOMA
WAKALA wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) imeeleza kuwa imejipanga kutoa Mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa Shule kwa Walimu Wakuu wapatao 17,000,kutoa mafunzo ya utawala Bora kwa wasimamizi wa elimu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
“Wakala umetoa mafunzo ya muda mfupi kuhusu uthibiti ubora wa shule wa ndani kwa walimu 7,612 ili kuwajengea uwezo wa kusimamia ufundishaji na ujifunzaji katika shule wanazosimamia,”amesema Dkt.Mgullah
Dkt.Mgullah pia ameelezea malengo ya wakala huo kwa mwaka 2022/2023 ambapo amesema kuwa wamedahili Walimu 2343 katika Kozi za CELMA, DEMA na DSQA, kuandaa Kiongozi cha Mwalimu Mkuu na kuandaa Mwongozo wa Utawala Bora kwa viongozi wa Serikali za Mitaa.
Kwa upande wake Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari-MAELEZO Bw. Gerson Msigwa amesema kuwa Serikali imeweka fedha nyingi kwenye sekta ya elimu nchi nzima ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/23, sekta ya elimu pekee imetengewa Shilingi trilioni 5.8. Chuo hiki ni moja ya juhudi za Serikali za kusimamia ubora wa elimu.
“Fedha hizi ni nyingi ambazo zinahitaji usimamizi wa karibu, hivyo wale viongozi wa kwenye taasisi zinazosimamia elimu lazima wawe na ujuzi na mbinu nzuri za kusimamia maendeleo ya elimu ili tuweze kupata thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali,
“Viongozi wanaosimamia Taasisi za Elimu wanatakiwa wakasome katika chuo hiki ili wakapate ujuzi wakasimamie vizuri taasisi hizo. Natoa wito kwa waajiri kutosita kuwaruhusu viongozi wa taasisi za elimu kwenda kusoma ADEM,”amesema Msigwa.