Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MWENYEKITI wa CCM wa Wilaya ya Simanjiro, Mkoani Manyara, Kiria Ormemei Laizer amesema Mwenyekiti Mtendaji wa shirika la ECLAT Foundation, Peter Toima amefanya mambo makubwa mno kuliko mwanasiasa yeyote Wilaya ya Simanjiro hivyo anapaswa kuungwa mkono.
Kiria ameyasema hayo kwenye tafrija iliyofanyika nyumbani kwake Kata ya Naisinyai baada ya kumshukuru Mungu katika Kanisa la KKKT kutokana na kuchagulikwa kuwa Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya hiyo hivi karibuni.
Amesema katika nguli wote wa siasa wa Wilaya ya Simanjiro hakuna mwanasiasa aliyefanya mambo makubwa ya maendeleo zaidi ya Toima hivyo aungwe mkono na siyo kubezwa.
Amesema Toima amefanya mambo mengi kwenye jamii nchini kwani amewezesha ujenzi wa shule zaidi ya 40 Tanzania hivyo kusaidia watoto wa jamii hasa za wafugaji kupata elimu.
“Hakuna mwanasiasa Simanjiro amefanya mambo makubwa kama Toima hivyo wananchi wa mkoa wa Manyara wanapaswa kumuunga mkono mwana maendeleo huyu na siyo kumbeza,” amesema Kiria.
Amesema kuna kipindi Toima aligombea ubunge kwenye jimbo la Simanjiro na baadhi ya wanasiasa wakawa wanambeza kuwa madarasa aliyojenga na wanafunzi wanaosoma waje kumpigia kura.
“Nilitoa machozi kwa uchungu mara baada ya kusikia baadhi ya wanasiasa wenye firka finyu wanabeza maendeleo ya mzee Toima badala ya kumpongeza na kumuunga mkono,” amesema Kiria.
Amesema kwenye kipindi chake cha uongozi wa CCM Wilaya ya Simanjiro atawaunga mkono wadau wote wanaofanya maendeleo kwenye eneo hilo.
“Ninatambua mchango wa mkurugenzi wa Ilaramatak marehemu Martin Ole Sanago ambaye alikuwa na miradi mingi na kutoa ajira zaidi ya vijana 1,000 ila wanasiasa wakamfitini,” amesema Toima.
Amesema pia akiwa kiongozi wa CCM atamuunga mkono mwekezaji mwingine Edward Laure ambaye ni mwana Simanjiro mpenda maendeleo anayehudumia jamii yaeneo hilo.
Diwani wa Kata ya Ngorika Albert Msole amesema wana CCM wa wilaya hiyo wapo tayari kumsaidia Mwenyekiti wao Kiria kufanikisha maendeleo ya Simanjiro kwani ni kijana msomi mwenye maono.
Diwani wa Kata ya Loiborsiret Ezekiel Lesenga (Mardadi) amempongeza Kiria kwa namna anavyokiunganisha chama chao japokuwa ana muda mchache tangu achaguliwe.
Diwani wa Kata ya Terrat Jackson Ole Materi amesema wana Simanjiro wakimpa ushirikiano Mwenyekiti wao watapiga hatua kubwa ya maendeleo, mshikamano na upendo.