Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas akimkabidhi rasmi Kamishina Mwandamizi wa TAWA Kanda ya Kusini Mashariki Abrah Juuru hati ya umiliki wa hifadhi ya Mbambabay yenye ukubwa wa hekari 597 ikijumuisha visiwa viwili ,milima na sehemu ya maji ya ziwa Nyasa. katika hafla iliyofanyika Mbambabay wilayani Nyasa
Kisiwa cha Lundo ambacho tayari TAWA wameanza uwekezaji wa wanyamapori jamii ya swala na ndege.
***************************
Serikali mkoani Ruvuma kwa kutambua umuhimu wa uhifadhi umewakabidhi Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) hati ya kukabidhiwa visiwa vya Lundo,Mbambabay na milima ya Mbamba na tumbi,yenye jumla ya hekari 597 kwa ajili ya uhifadhi.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amekabidhi hati ya kumilikishwa eneo hilo ambapo pia amezindua uwekezaji wanyamapori katika kisiwa cha Lundo ambapo tayari wamewekwa wanyamapori jamii ya swala na ndege.
Kanali Laban amesisitiza kuwa kupelekwa kwa wanyama katika kisiwa hicho,kutasaidia kuongeza vivutio kwa watalii kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana wilaya ya Nyasa na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla
Mkuu wa Mkoa amewaagiza wadau wa utalii na uhifadhi wakiwemo TAWA na TANAPA kuchukua jukumu la kutoa elimu ya uhifadhi na utalii kwa wananchi hasa wa Mkoa wa Ruvuma kuhusu umuhimu wa sekta ya utalii katika kuchochea uchumi sanjari na kufungua vituo vya utoaji taarifa za utalii katika kila Halmashauri.
Akizungumzia historia ya kivutio cha utalii ambacho ni kisiwa cha Lundo chenye ukubwa za hekta 20,Mganga Mkuu Mstaafu wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa Dk.John Paparika ambaye pia wazazi wake wametokea katika Kisiwa hicho anasema kisiwa kimepewa jina la Lundo kwa sababu watu wa kwanza waliovuka kisiwa hicho kwenda ng’ambo ya pili walifikia kijiji cha Lundo.
Anasema kisiwa hicho tangu zamani kilikuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa vijiji vya Lundo,Ngindo na Chinula kwa sababu wakati wa vita ya Majimaji vilivyotokea kati ya mwaka 1905 hadi 1907 watu walikuwa wanakimbilia katika kisiwa hicho ambacho kina maeneo ya maficho.
“Baada ya vita ya Majimaji kuanzia mwaka 1908 kisiwa hiki kilitumika na wakoloni wa kijerumani kuwahifadhi watu waliopata ulemavu kutokana na ugonjwa wa ukoma ambao baadaye walihamishiwa katika kisiwa cha Puulu’’,anasema Dk.Paparika.
Hata hivyo anasema watu hao wenye ukoma walipandiwa matunda ya aina mbalimbali katika kisiwa hicho yakiwemo maembe, mapera,mananasi,machungwa na migomba ambapo hadi sasa katika kisiwa hicho kuna masalia ya miembe mingi na makaburi.
Anasema licha ya watu hao wenye ukoma kutengwa katika kisiwa hicho ,bado ndugu zao kila wiki walikuwa wanafika katika kisiwa hicho kuwatembelea na kuwaletea vyakula kwa kuwa kutokana na ulemavu waliopata walikuwa hawawezi kufanyakazi hivyo walihitaji msaada.
Historia ya kisiwa hicho,inaonesha kuwa kisiwa kilisaidia wakati wa mgogoro wa kutoelewana baina ya kabila la wamatengo wa Wilaya ya Mbinga na Wanyasa wa Mwambao mwa ziwa Nyasa ambapo wamatengo walipokuwa wanashuka na silaha zao wakazi wa kata za Lundo na Mbambabay walikuwa wanakimbilia kujificha katika kisiwa hicho.
“Kwa kuwa wamatengo hawana uwezo wa kuogelea wala kuendesha mitumbwi,hivyo walikuwa wanashindwa kuwapata wanyasa ambao walikuwa wanapiga kasia na kujificha katika kisiwa cha Lundo’’,anasema Dk.Paparika.
Anasema kisiwa hicho kina utajiri wa aina mbalimbali za samaki wa mapambo ambao wanapenda kuishi sehemu za mawe.Inakadiriwa samaki mmoja wa mapambo katika nchi za Ufaransa,Ujerumani na Afrika ya Kusini anauzwa kati ya dola za Marekani 400 hadi 500 sawa na zaidi ya sh.milioni moja kwa samaki mmoja.
Mshauri wa Maliasili na Utalii Mkoa wa Ruvuma Afrikanus Challe anasema hifadhi ya Mbambabay ina ukubwa wa eneo la hekta 597 na kwamba maeneo hayo yanafaa kwa kufuga wanyamapori na ndege.
Hata hivyo anasema Kati ya hekta hizo, mlima Mbamba una eneo lenye ukubwa wa hekta40,mlima Tumbi hekta 110,kisiwa Mbambabay kina hekta 27, kisiwa cha Lundo kina ukubwa wa hekta 20.
“Milima na visiwa hivi vimejaaliwa kuwa na uoto mzuri wa miombo,mawe yanayozunguka visiwa hivi na milima kando kando ya ziwa yana hifadhi samaki adimu wa mapambo zaidi ya aina 400’’,anasisitiza Challe.
Kwa mujibu wa Challe,eneo la hifadhi ya Mbambabay ni muhimu sana kwa upande wa Tanzania hususan katika matumizi ya shughuli za utalii kama vile utalii wa kuvua samaki,kupiga mbizi,yatching,utalii wa kuendesha mitumbwi na kuweka kambi kwenye fukwe.
Mtalaam huyo wa uhifadhi anasema eneo hilo likihifadhiwa litatumika kwa ajili ya mazalia ya samaki na hivyo kuongeza kipato kwa wananchi wanaotegemea shughuli za uvuvi.
“Mbambabay ikihifadhiwa inaweza kuleta ushindani kibiashara kwa sababu katika nchi yetu hakuna eneo linaloweza kutoa mchanganyiko mzuri wa huduma za kitalii kama zitakazotolewa katika eneo hili’’,anasisitiza Challe.
Wilaya ya Nyasa inaongoza katika Mkoa wa Ruvuma kwa kuwa na vivutio vya aina mbalimbali vya utalii.