Na. WAF – Mwanza
Katika kipindi cha miaka 20 toka mwaka 2013 gharama zitokanazo na magonjwa yasiyoambukiza zinafikia Dola za Marekani trilioni 47, fedha ambazo zingeweza kutumika kupunguza umaskini Duniani kwa watu bilioni 2.5 kwa miaka 50.
Hayo yamesemwa leo na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana kwenye kilele cha maadhimisho ya kitaifa ya wiki ya kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza na uzinduzi wa mkakati wa Taifa wa kuzuia magonjwa hayo.
“Taarifa za mwaka 2013 za Shirika la Maendeleo Duniani (UNDP) zinaonesha kuwa, pamoja na changamoto za kiafya, magonjwa yasiyoambukiza yanaathiri sana nyanja mbalimbali za maisha kwa kutojiongezea kipato kwa jamii na nchi kwa ujumla.” Amesema Bw. Elikana
Akiendelea kutoa ufafanuzi huo Bw. Elikana amesema kuwa nchi za uchumi wa kati na chini, magonjwa haya yatayagharimu mataifa hayo jumla ya Dola za Marekani trilioni 7 kwenye kipindi cha 2011-2025.
Makadirio yanaonesha kuwa gharama za huduma kwa magonjwa yasiyoambukiza itafikia asilimia 75 ya mzigo wote wa bajeti ya afya, huku ugonjwa wa kisukari pekee ukipelekea gharama ya zaidi ya Dola za Marekani bilioni 465 sawa na asilimia 11 ya bajeti yote ya afya duniani.
“Magonjwa yasiyoambukiza yalikuwa yanachangia asilimia 20 tu miaka ya 90 lakini kwa sasa yanachangia asilimia 33 kwa takwimu za mwaka 2016, na kwa sasa inakadiriwa yanaweza kufikia hadi asilimia 40 katika baadhi ya maeneo nchini Tanzania.” Amesema Bw. Elikana
“Nitoe wito kwa Wizara zote kuhakikisha zinaandaa mikakati na mipango ya utekelezaji kwa ajili ya kutekeleza afua mbalimbali za kukinga na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza katika maeneo yao.” Amesema Bw. Elikana ambae alikua mgeni rasmi kwenye kilele hicho
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Prof. Paschal Ruggajo amesema maadhimisho haya yanafanyika kwa mara ya nne hapa nchini yakihusisha tamasha la michezo na mazoezi ya mwili, Kongamano la Kisayansi, Maonesho ya wadau mbalimbali na upimaji wa Afya bure kwa wananchi.
“Dhumuni la shughuli hizo zote ni kuleta matokeo chanya kwenye mipango ya Serikali na kutengeza mikakati endelevu ya kuzuia na kudhibiti Magonjwa yasiyoambukiza.” Amesema Prof. Ruggajo
Akitolea mfano kwenye michezo Prof. Ruggajo amewahamasisha wananchi kujenga tabia na kuwa na hamasa ya kufanya mazoezi ili kudhibiti Magonjwa Yasioambukiza.
Pia, amesema wananchi wanatakiwa kujenga tabia ya kupima afya mara kwa mara ili kudhibiti na kukinga Magonjwa Yasiyoambukiza nchini na kupelekea kupata fedha za maendeleo na sio fedha za kutibu magonjwa hayo.