Rais wa Bunge la Afrika (Pan African Parliament – PAP), Mhe. Chifu Fortune Charumbira akihutubia wakati akifunga Mkutano wa kwanza wa kawaida wa Bunge la Sita la Afrika (Pan African Parliament – PAP), umefungwa leo Alhamisi Novemba 10,2022 katika ukumbi wa Bunge la Afrika, Midrand Afrika Kusini. Picha na Kadama Malunde
Rais wa Bunge la Afrika (Pan African Parliament – PAP), Mhe. Chifu Fortune Charumbira akihutubia wakati akifunga Mkutano wa kwanza wa kawaida wa Bunge la Sita la Afrika (Pan African Parliament – PAP), umefungwa leo Alhamisi Novemba 10,2022 katika ukumbi wa Bunge la Afrika, Midrand Afrika Kusini.
Rais wa Bunge la Afrika (Pan African Parliament – PAP), Mhe. Chifu Fortune Charumbira akihutubia wakati akifunga Mkutano wa kwanza wa kawaida wa Bunge la Sita la Afrika (Pan African Parliament – PAP), umefungwa leo Alhamisi Novemba 10,2022 katika ukumbi wa Bunge la Afrika, Midrand Afrika Kusini.
Rais wa Bunge la Afrika (Pan African Parliament – PAP), Mhe. Chifu Fortune Charumbira akihutubia wakati akifunga Mkutano wa kwanza wa kawaida wa Bunge la Sita la Afrika
Na Kadama Malunde- Midrand Afrika Kusini
Rais wa Bunge la Afrika (Pan African Parliament – PAP), Mhe. Chifu Fortune Charumbira amefunga Mkutano wa kwanza wa kawaida wa Bunge la Sita la Afrika (Pan African Parliament – PAP) leo Alhamisi Novemba 10,2022 katika ukumbi wa Bunge la Afrika, Midrand Afrika Kusini.
Mkutano wa Kwanza wa kawaida wa Bunge la Sita la Afrika ulioanza Oktoba 24,2022 na kuhitimishwa leo Alhamisi Novemba 10,2022 uliongozwa na Kauli mbiu ya Afrika ya mwaka 2022 ‘Kujenga Ustahimilivu kwenye lishe Afrika : Kuharakisha maendeleo ya mtaji wa kibinadamu, kijamii na kiuchumi’.
Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo, Rais wa PAP, Chifu Fortune Charumbira amesema maazimio yote yaliyofikiwa yatafikishwa kwa viongozi wa nchi za Afrika zinazohusika na kwamba kilichobaki sasa ni kutekeleza maazimio yaliyofikiwa na wabunge wa Bunge la Afrika.
Yafuatayo ni Sehemu ya Maazimio ya Mkutano wa Kwanza wa kawaida wa Bunge la Sita la Afrika uliofanyika Oktoba 24,2022 hadi Alhamisi Novemba 10,2022
MRADI WA MAFUTA TANZANIA NA UGANDA
Miongoni mwa maazimio ya Mkutano huo wa Bunge la Afrika Kuhusu Azimio la Bunge la Ulaya kuhusu Uganda na Tanzania linalohusishwa na uwekezaji katika mradi wa Mafuta ghafi, Bunge la Afrika ambapo wabunge wameafiki kuwa Azimio kama hilo linakiuka uhuru wa Uganda na Tanzania ikizingatiwa kuwa Afrika inahitaji kuendeleza rasilimali zake ikiwa ni pamoja na mafuta na gesi ili kupambana na nishati na umaskini wa kiuchumi.
Hivyo Bunge la Afrika linaunga mkono Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi Afrika Mashariki hivyo kuazimia kuunga mkono haki za mataifa ya Afrika Kuendeleza rasilimali zao za mafuta na gesi ili kuziwezesha kujenga ustahimilivu na kufadhili ajenda yao dhidi ya mabadiliko ya Nishati.
Aidha Bunge limesisitiza ukweli kwamba Afrika na nchi nyingine zinazoendelea lazima ziwe na ajenda tofauti ya mabadiliko ambayo yanaziruhusu kuendeleza rasilimali zao ili kushughulikia masuala yao ya kimaendeleo yanayowakabili ili kuondoa umaskini na kuboresha ustahimilivu.
Aidha kwa kutambua hitaji la jamii ya Kiafrika kupata teknolojia ili kusaidia maendeleo ya masuluhisho ya nishati jadidifu katika bara la Afrika pia kuzisaidia Uganda na Tanzania katika mradi wao wa Bomba la mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) pamoja na kusisitiza haja ya nchi zote za Afrika kuzingatia haki za binadamu za watu wote na kupeleka azimio hili kwenye mabunge yao ya taifa.
Wabunge wakiwa ukumbini
KUHUSU AZIMIO LA MSHIKAMANO NA KUUNGA MKONO SERIKALI NA WANANCHI WA JAMHURI YA MSUMBIJI
Bunge la Afrika linapinga vikali na kulaani vitendo vya kinyama, vya kutisha na vya uoga vinavyofanywa na magaidi dhidi ya watu wa Msumbiji hususani wanawake na watoto na wazee tangu mwaka 2017 na kusababisha vifo zaidi ya 2000 na watu zaidi ya laki sita kukimbia makazi yao.
Pia Bunge limelaani wale wanaofadhili, kutoa silaha na kuchochea ugaidi na misimamo mikali nchini Msumbiji na Afrika kwa ujumla na kwamba linatoa rambirambi za dhati kwa serikali ya Watu wa Msumbiji na nchi nyinginezo barani Afrika na waathirika wa vitendo vya kigaidi.
Aidha Bunge la Afrika linahimiza Wakuu wa Nchi na Serikali za Afrika kuendelea kufanya kazi kwa bidii katika kuisaidia Serikali na Wananchi wa Msumbiji katika kupambana na janga la ugaidi na misimamo mikali inayotishia kuathiri ukanda mzima wa SADC.
Mkutano wa bunge ukiendelea
VIKWAZO VYA KIUCHUMI VILIVYOWEKWA KWA SERIKALI YA ZIMBABWE NA MAREKANI, UINGEREZA NA UMOJA WA ULAYA.
Bunge la Afrika limetoa wito wa kuondolewa mara moja kwa vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na Marekani, Uingereza na Umoja wa Ulaya dhidi ya Serikali na Watu wa Zimbabwe ambapo kuondolewa kwa vikwazo hivyo vya kiuchumi kutaiwezesha Serikali ya Zimbabwe kuvutia uwekezaji wa Moja kwa moja wa Kigeni ambao utakuwa chachu ya kufufua uchumi ambao unahitajika sana kukidhi matarajio ya wananchi wake.
MKATABA WA AFRIKA KUHUSU HAKI ZA BINADAMU KUHUSIANA NA HAKI ZA WANAWAKE AFRIKA (INAYOITWA PROTOKALI YA MAPUTO).
Bunge la Afrika linaunga mkono Ushiriki wa Kamati ya wanawake katika mchakato wa kuandaa makataba kuhusu Unyanyasaji dhidi ya wanawake utakaoandaliwa baadaye, Kampeni yake ya kuridhia katika ngazi ya kitaifa na kuenezwa kwake.
Pia Bunge la Afrika linaunga mkono Kampeni ya ‘Siku 16 za Uanaharakati’ dhidi ya ukatili wa kijinsia kuanzia tarehe 25 Novemba, Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na kuendelea hadi tarehe 10 Desemba, Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu.
Wabunge wakiwa ukumbini
UHAMIAJI WA KUTAFUTA KAZI BARANI AFRIKA
Bunge la Afrika limeidhinisha Ombi lililotolewa na Kamati ya Kudumu ya Biashara, Forodha na Uhamiaji la kutunga sheria ya mfano kuhusu uhamiaji wa kutafuta kazi barani Afrika, kuimarisha ulinzi wa kazi ya wafanyakazi wahamiaji,kuendeleza Mikataba ya Uhamiaji wa kutafuta kazi baina ya nchi mbili (BLMAs) na kuongeza ulinzi wa kijamii kwa wafanyakazi wahamiaji barani Afrika.
ENEO HURU LA BIASHARA BARANI AFRIKA (AfCFTA)
Bunge la Afrika limewaomba Wabunge wa mabunge ya nchi za Afrika ambazo hazijaridhia Mkataba wa AfCFTA kuongeza kujenga uelewa miongoni mwa serikali zao ili kuridhia Mkataba na kuwaomba wabunge kuhamasisha nchi zao kusaini na kuridhia pale inapofaa, Protokali ya Mkataba uliyoanzisha Jumuiya ya Uchumi ya Kanda Afrika inayohusiana na Watu Kusafiri kwa Uhuru, Haki ya ukaazi na haki ya kuanzisha makazi.
SHERIA YA MFANO KUHUSU USALAMA WA CHAKULA NA LISHE AFRIKA
Bunge la Afrika limeazimia kupitisha Sheria ya Mfano ya Usalama wa Chakula na Lishe Barani Afrika na kuiomba kamati ya Uchumi wa Vijijini, Kilimo, Maliasili na Mazingira na Umoja wa Mabunge ya Afrika (Pan African Parliamentary Alliance) kuendelea na uhamasishaji na mipango mingine ya chakula na usalama na kuimarisha uwezo wa wabunge barani Afrika kwa ajili ya kuweka mazingira wezeshi ya usalama wa chakula na lishe ikiwemo haki ya kupata chakula cha kutosha barani Afrika.
Wabunge wakiwa ukumbini
SHERIA YA MFANO KUHUSU POLISI AFRIKA
Bunge la Afrika limetoa Wito kwa Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (UA) kupitia upya sheria zao za Polisi na Sheria ya mfano ya Polisi kwa Afrika na kufanya marekebisho yote yanayohitajika kwa sheria zao ili kukuza uwiano na sheria ya mfano.
KUHIMIZA URIDHIAJI WA PROTOKALI YA WATU WENYE ULEMAVU NA PROTOKALI YA WAZEE
Bunge limeazimia kuongeza uhamasishaji wa Kibunge na Ushirikishaji wa uridhiaji, utumikaji katika nchi na utekelezaji wa Protokali ya Mkataba wa Afrika wa haki za binadamu kuhusu watu wenye ulemavu na kueneza kwa umma sheria ya mfano ya ulemavu iliyopitishwa na Bunge.
SHERIA KUHUSU USHIKIKA BARANI AFRIKA
Bunge limependeza kutungwa kwa sheria la Mfano ya Sheria ya Vyama vya Ushirika Barani Afrika
KUHUSU UHIMIZAJI WA MPANGO WA UTEKELEZAJI WA MIAKA 10 YA KUTOKOMEZA AJIRA YA WATOTO,KAZI ZA KULAZIMISHWA, USAFIRISHAJI HARAMU WA BINADAMU NA UTUMWA WA ZAMA ZA KISASA(2020-2030).
Bunge la Afrika limependekeza kuongeza ushawishi wa Bunge na uhusikaji katika uridhiaji, utumikaji katika nchi na utekelezaji wa Protokali ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu kuhusu haki na ustawi wa mtoto ili kuhakikisha ulinzi wa haki zao na ukuaji.
MAPENDEKEZO YA MJADALA 2022 WA VIONGOZI WA JUU WA BUNGE KUHUSU DEMOKRASIA, HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA KATIKA AFRIKA CHINI YA MADA YA MABADILIKO YA SERIKALI YASIYOFUATA KATIBA NA MAGEUZI YA KISIASA KATIKA AFRIKA
Bunge la Afrika limeazimia kulaani Majeshi yote ya nje yanayochochea migogoro barani Afrika, katika nchi kama vile Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Msumbiji na Ukanda wa Sahel na kuhakikisha kunaanzishwa kwa mkakati ulioratibiwa wa ufuatiliaji na uingiliaji kati wa mapema ili kutambua nchi zinazoweza kukumbwa na Mapinduzi na kuingilia kati ili kuzuia mapinduzi hayo zaidi ya kushirikishana taarifa nan chi wanachama na matarajio kwamba Jumuiya za Kiuchumi za Kikanda zinapaswa kuongoza.
Aidha Bunge la Afrika limetoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (UA) kuridhia hati za Kisheria za Umoja wa Afrika hasa Protokali ya Malabo.
Hali kadhalika Bunge la Afrika limeutaka Umoja wa Afrika kuunda Jeshi la Afrika kama Jeshi la kudumu ili kuingilia kati kutatua migogoro ikiwemo mabadiliko ya serikali yasiyofuata katiba pamoja na kuutaka Umoja wa Afrika kuunda Mahakama ya Jinai ya Afrika kwa kuongeza muda wa mahakama ya Afrika kuwahukumu wahusika wa uhalifu dhidi ya binadamu.
Pia Bunge la Afrika kuhamasisha Kupitishwa kwa Sheria za Umoja wa Afrika (UA) zinazokataza mabadiliko ya serikali yasiyofuata katiba pamoja na kuendeleza Demokrasia na Utawala wa Sheria sambamba na kuzitaka nchi wanachama kuimarisha taasisi za utawala na taratibu za uwajibikaji wa kitaifa ili kuruhusu umma kwa ujumla kuwajibisha serikali na kudai mageuzi kama njia ya kuhakikisha kuwa serikali zinaaminiwa na raia.
Bunge hilo pia limetoa wito kwa Wakuu wan chi za Umoja wa Afrika kuthibitisha hadi yao katika ngazi ya bara kupitia uridhiaji wa sheria na hatua za haraka katika kushughulikia mabadiliko ya serikali yasiyofuata katiba.
Wabunge wakiwa ukumbini
MAPENDEKEZO YA MKUTANO WA 13 KUHUSU HAKI ZA WANAWAKE
Bunge la Afrika limetoa wito kwa Serikali na mabunge kuweka kipaumbele katika uandaaji wa mipango kazi ya kitaifa inayoshughulikia uelewa wa ukatili dhidi ya wanawake na wasichana katika mikakati yao ya kitaifa na kuyafikia malengo ya maendeleo endelevu na Ajenda ya Umoja wa Afrika (UA) ambapo Bunge la Afrika na asasi zinatakiwa kufuatilia utekelezaji wa ahadi za kitaifa.
Bunge la Afrika limewataka Wanawake wote wa Afrika kuhamasishana ili kujitangaza kupitia vyombo vya habari popote walipo pamoja na Mabunge ya kitaifa yaimarishe na kukuza ushirikishwaji na ushiriki wa wanawake na vijana katika utungaji na utekelezaji wa sera na AfCFTA na kuendeleza afua zinazolenga biashara isiyo rasmi ya mipakani kwa nia ya kulinda biashara za wanawake na kuhimiza urasimishaji wao.
Bunge la Afrika pia limezitaka serikali kuanzisha Programu za mafunzo kwa wanawake na wajasiriamali vijana kuhusiana na matumizi ya zana za kidigitali na kutenga rasilimali zinazojumuisha teknolojia, majukwaa mapya ya vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na kuboresha upatikanaji wa ufadhili wa kibiashara kwa kutunga sheria za fedha zinazoendana na shughuli za kibiashara za wanawake na vijana.
Hali kadhalika Bunge la Afrika linazihimiza serikali kuongeza motisha kwa ajili ya ujumuishaji wa wanawake na vijana katika shughuli za ushirika na uchumi usio rasmi katika maeneo ya vijijini sambamba na kuwataka wabunge kuzitaka serikali zao kuharakisha mchakato wa kutia saini, kuridhia na kutekeleza taratibu za utumikaji wa Protokali ya Maputo.
Picha zote na Kadama Malunde – Malunde 1 blog Midrand Afrika Kusini