Mkurugenzi Mkuu wa Floresta Tanzania, Richard Mhina.
*************
Na Selemani Msuya, Dodom
SHIRIKA la Floresta Tanzania kwa kushirikiana vikundi zaidi ya 500 vya uhifadhi wa mazingira mkoani Kilimanjaro, wanatarajia kupanda miti 700,000 katika kipindi cha mwezi Novemba na Desemba 2022, ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Richard Mhina wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii jijini hapa, ambapo anashiriki kongamano la wadau wa mbegu asili na zilizosahaulika.
Mhina alisema shirika hilo limekuwa na kampeni kila mwaka mara mbili, ambapo wanatumia kipindi cha masika na vuli kupanda miti hiyo.
“Kuanzia mwezi huu hadi Desemba tunatarajia kupanda miti 700,000 katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo, hasa kandokando ya Mlima Kilimanjaro, ili kuwafanya wananchi wanaoshi maeneo hayo wasiharibu msitu,” alisema.
Alisema awamu ya kwanza wamepanda miti 800,000 hivyo kufikisha lengo la kila mwaka kupatanda miti milioni 1.5.
“Kila mwaka tunajipangia kupanda miti milioni 1.5, ambapo masika tunapanda miti 800,000 na vuli miti 700,000 zoezi ambalo litafanyika mwezi huu na Desemba,” alisema.
Alisema utafiti unaonesha kuwa kati ya vikundi 500 vyenye wanachama zaidi ya 15,000 kila kikundi kinaweza kuzalisha miche zaidi 2,000.
Mhina alisema miti mingi inaoteshwa pembezoni mwa Mlima Kilimanjaro na vyanzo vya maji vilivyopo katika mkoa huo, ili kuhakikisha mazingira yanatunzwa na kuendelezwa.
Alisema kasi ya mabadiliko ya tabianchi imekuwa ikiongezeka kila siku, hivyo njia ya kukabiliana na hali hiyo ni kuhakikisha miti inapadwa kila kona ya mkoa na nchi kwa ujumla.
“Tunafanya shughuli nyingi za uhifadhi wa mazingira mkoani Kilimanjaro, moja ya mbinu tunayotumia ni kutoa elimu na kuunda vikundi vya kuweka na kukopa vinapewa elimu ya kuanzisha vitalu vya miti ambayo inatumika kupandwa kwenye vyanzo vya maji, mashambani na pembezoni kwa Mlima Kilimanjaro,” alisema.
Aidha, Mkurugenzi alisema moto ambao umetokea Mlima Kilimanjaro unaweza kuleta madhara katika miaka ijayo, hasa kwa kupoteza uasili wake, hivyo kuikosesha serikali mapato ya utalii.
Aliiomba Serikali kuchunguza kwa kina chanzo cha moto huo, ambao umeweza kuleta madhara makubwa katika mlima huo muhimu katika sekta ya utalii na uchumi kwa ujumla.
Akizungumzia kongamano la mbegu asili na zilizosahaulika, alisema limefanyika wakati muafaka hasa ikizingatiwa kuwa kumekuwepo na nguvu kubwa ya kuingiza mbegu za viwandani katika kilimo, hivyo kuzifanya mbegu asili kusahaulika.
“Tukumbuke kuwa mbegu ndio chakula na kwa sasa makampuni makubwa ndiyo yenye nguvu katikaeneo hilo na kufanya mbegu asili na haki za mkulima zinalindwa,” alisema.
Mhina alisema kongamano hilo la wadau wa kilimo hai na mbegu asili limeangalia maslahi ya taifa zaidi kwa miaka ijayo, ili isije kutokea mbegu asili zinapotea kwenye kilimo.
Alisema mbegu asili zina sifa ya kutunza mazingira, hivyo serikali haina budi kuhakikisha sera na sheria zinalinda mbegu hizo na mkulima kwa ujumla.
“Kuna vita ya Ukraine na Urusi, iwapo nchi hizo ambazo zinasifika kwa kilimo, iwapo zitazuia mbegu kutoka madhara yake ni makubwa, hivyo sisi tunasisitiza serikali iangalie eneo la mbegu asili kwa mustakabali wa kilimo chetu,” alisema.