HOFU pamoja na ukosefu wa bajeti ndani ya vyombo vya habari,imebainika kuwa kikwazo kwa baadhi ya Waandishi kutojihusisha na uandishi wa habari za uchunguzi zitakazoweza kuibua mambo mbalimbali yanayoikabili jamii ikiwemo Uhuru wa kujieleza.
Hayo yamebainika katika mafunzo ya siku tatu (3) yaliyoandaliwa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika,Tawi la Tanzania (MISA-TAN) kuwajengea uwezo wa kutafuta na kuchakata habari zitakazo chochea Uhuru wa kujieleza kwa Wanahabari zaidi ya 40 kutoka Mikoa ya Tabora, Dodoma, Shinyanga, Simiyu na wenyeji mkoa wa Singida.
Baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa na Waandishi washiriki katika mafunzo ni kuwataka uta wamiliki wa vyombo vya habari kutenga bajeti kwa Waandishi kuzalisha vipindi vyenye ubora ili kuchochea habari za uchunguzi na uhuru wa kujieleza.
“Waandishi wengi hawafanyi habari za Uchunguzi na Uhuru wa kujieleza kwa sababu ya ufinyu wa bajeti katika vyombo vyetu vya habari ili kuwezesha ukusanyaji ya taarifa ikizingatiwa kuwa uandishi wa habari za uchunguzi ni za muda mrefu na zinahitaji gharama ili kukamilisha” alisema Samira mshiriki na mwandishi wa habari kutoka mkoani Simiyu.
Ameendelea kusema kwamba waandishi wa habari Tanzania wana uhuru kuchapisha lakini hofu hutanda baada ya andiko hilo kuonekana kwenda kinyume na matakwa ya watu au taasisi husika hali iliyopelekea kuzaliwa kwa mifumo kandamizi katika sekta ya habari.
“KWA MUJIBU WA SHERIA ILIYOPO SASA NI RAHISI KOSA LA KITAALUMA KUGEUKA JINAI NA MWANDISHI AKAWAJIBISHWA HILO PIA LINACHOCHEA WAANDISHI KUKAA KIMYA.”amesema.
Kwa upande wake Mwezeshaji wa Mafunzo hayo Marko Gideon, amesema Wanahabari wanapaswa kutumia kalamu zao vyema kuandika habari za uhuru wa kujieleza katika Nyanja mbalimbali ili kupaza sauti za wananchi ambao kwa kiasi kikubwa wanategemea vyombo vya habari kufikisha vilio vyao.
Bw.Gideon kwamba Uhuru wa Kujieleza ni moja ya nguzo katika kujenga msingi imara Utawala wa bora kwa vile wananchi wote watashiriki katika kutoa maoni kwa ujenzi wa mambo mbalimbali katika taifa.
“NCHI ISIYO NA UHURU WA KUJIELEZA HAUTAKUWEPO UWAJIBIKAJI KWA VIONGOZI, HAKUTAKUWA NA USAWA WA KISHERIA, HAKUNA UWAZI, UCHAGUZI HAUWEZI KUWA HURU NA HAKI, WALA KUDHIBITI MATUMIZI MABAYA MADARAKA KWA VIONGOZI” amesema Bwana Gideon.
Naye Andrew Marawiti kutoka Misa-Tan, amesema lengo kuu la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo waandishi wa habari ili kuzalisha maudhui yenye ubora yanayohusiana na Uhuru wa Kujieleza.