*********
NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Ndaki ya Sayansi za Jamii wameandaa Kongamano la Kimataifa linalohusu Sauti ya Wanasayansi za Jamii ambalo litafanyika Novemba 10 hadi 11, 2022 katika Kampasi ya Mwalimu Nyerere, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Akizungumza na Waandishi wa habari leo Novemba 7,2022 Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti Kamati ya Maandalizi Dkt.Muhidin Shangwe amesema kongamano la mwaka huu linaleta wataalamu wa sayansi za Jamii wapatao 200 kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika ili kujadili mienendo ya mabadiliko yanayojitokeza barani Afrika na kwingineko kwenye nchi za Kusini mwa Dunia.
“Kongamano la 7 la Sauti ya Sayansi ya Jamii (VSS2022) linakusudia kupaza sauti za wanataaluma wa Sayansi za Jamii kuhusu mabadiliko yanayoendelea kutokea Duniani na athari zake hususan Kusini mwa Dunia”. Amesema
Amesema katika Kongamano hilo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo-UTAFITI, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof.Bernadeta Killian.