Muonekano wa barabara ya Muhutwe-Kamachumu-Muleba KM 52 ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami unaendelea mkoani Kagera.
Muonekano wa barabara ya Kanyambogo –Rubya-Ibuga KM 3.5 ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami unaendelea mkoani Kagera.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi), Mhe. Elius John Kwandikwa akiongoza timu yake kuvuka daraja la muda wakati alipokagua ujenzi wa daraja la kudumu la Kitengule linalounganisha wilaya za Karagwe na Misenyi mkoani Kagera, daraja hilo lina urefu wa mita 140.
Mhandisi mshauri Eng. Lucas Nyaki anayesimamia ujenzi wa daraja la Kitenguie akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi), Mhe. Elius John Kwandikwa alipokagua ujenzi wa daraja hilo linalounganisha wilaya za Karagwe na Misenyi mkoani Kagera.
Muonekano wa nguzo ya msingi wa daraja la Kitengule lenye urefu wa mita 140 linalojengwa ili kuunganisha wilaya za Karagwe na Misenyi mkoani Kagera .
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi), Mhe. Elius John Kwandikwa akifafanua jambo kwa timu ya mkandarasi na msimamizi wa ujenzi wa daraja la Kitengule mkoani Kagera.
………………..
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (sekta ya ujenzi), Mhe. Elius John Kwandikwa amemtaka mkandarasi CHICO anayejenga daraja la Kitengule lenye urefu wa mita 140 na barabara unganishi yenye urefu wa KM 18 kukamilisha kazi hiyo kwa wakati na ubora unaotakiwa.
Amesema tayari Serikali imeshalipa madai ya mkandarasi yaliyohakikiwa hivyo ni wakati wa mkandarasi huyo kuongeza kasi ili kuepuka kisingizio vya mvua pindi itakapoanza kunyesha.
“Nimeridhika na kazi mnayoifanya ni nzuri hivyo ongezeni kasi bila kuathiri ubora,” amesisitiza Naibu Waziri Kwandikwa.
Amesema kuwa ukamilika kwa daraja la Kitengule na barabara unganishi kutaongeza tija katika shughuli za uzalishaji wa bidhaa za kilimo, mifugo na viwanda katika eneo hilo na kuchochea ukuaji wa uchumi wa wilaya za Karagwe na Misenyi.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Kagera Eng. Andrew Kasamwa amesisitiza kuwa yeye na timu yake wamejipanga kikamilifu kuhakikisha kasi na ubora katika ujenzi wa miradi yote ya barabara na madaraja mkoani Kagera inazingatiwa.
Aidha amemtaka mkandarasi JOSSAM anayejenga barabara ya Muhutwe-Kamachumu-Muleba KM 52 na Kanyambogo-Rubya-Ibuga KM 3.5 kuongeza kasi ya ujenzi na kuruhusu barabara hizo kutumika wakati ujenzi wake ukiendelea bila kuathiri shughuli za wananchi wilayani humo.
Naibu Waziri Kwandikwa yuko katika ziara ya siku tatu mkoani Kagera kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu.
Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano septemba 26, 2019.