Zaidi ya Wakulima 300 ambao ni wanachama wa chama cha Wakulima Tanganyika (TFA) kutoka mikoa mbali mbali ya Tanzania wameshiriki mkutano mkuu wa chama hicho ambao umejidili masuala mbali mbali ikiwemo upatikanaji wa pembejeo za bei nafuu pamoja na fursa za masoko ya ndani na nje ya nchi.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu , Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wakulima Tanganyika Justine Shirima amesema kuwa chama hicho kimefanya mauzo ya mazao ya wakulima yanayofikia bilioni 12 mpaka sasa.
Shirima amesema kuwa mbali na kutafuta masoko kwa mazao ya wakulima pia chama hicho kinawawezesha wakulima kupata pembejeo kwa bei nafuu.
“Tumetoka kutengeneza hasara sasa tunatengeneza faida kwa wanahisa wetu tunamatumaini makubwa na muda si mrefu tutatoa gawio ambalo tulikuwa hatujatoa kwa kipindi cha miaka mingi kwani kampuni ilikuwa inatengeneza hasara ikiwa kwa sasa inatengeneza faida,”Alisema Shirima.
Askedem Kaaya ni mwanachama katika chama hicho ameiomba serikali kuipa kibali TFA cha uwakala wa kusambaza pembejeo pamoja na kuwasimamia watendaji na viongozi wa chama hicho ipasavyo ili kutekeleza haki ya wanahisa.
“Changamoto kubwa kwa wakulima ni pembejeo ,zinakuja lakini zinakuwa na gharama kubwa na kusababisha wakulima wengi kutolima kutokana na kushindwa kupata pembejeo lakini pia hali ya mabadiliko ya tabia nchi hivyo tunaiomba serikali iweze kumsaidia mkulima kupata pembejeo kwa bei nafuu ili aweze kuzalisha zaidi,”Alisema Kaaya