NJOMBE
Serikali mkoani Njombe ikiongozwa na katibu tawala Judica Omary imefanya ukaguzi wa miradi 7 ya maendeleo inayotekelezwa katika kata tofauti za halmashauri ya wilaya ya Njombe kutoka sekta ya Afya,elimu pamoja na mradi wa jengo la utawala kisha kukiri kuridhishwa na ubora katika utekelezaji wake.
Licha ya kuridhishwa na mwenendo wa uetekelezaji wa miradi hiyo ya maendeleo lakini timu ya ukaguzi imebaini dosari ndogo za kiufundi kwa baadhi ya miradi ukiwemo wa zahanati ya Lole na kisha kutoa maagizo kwa wakandarasi kufanya marekebisho haraka
Mara baada ya kufanya ukaguzi wa miradi hiyo ndipo katibu tawala wa mkoa wa Njombe Judica Omary akatoa neno kwa wakandarasi ,wananchi na watalaamu wa serikali kuhakikisha wanashirikiana katika utekelezaji ili iane kutoa manufaa kwa jamii
Omary amesema serikali imedhamiria kuboresha huduma za jamii na kwamba itaendelea kutoa fedha kwa ajili ujenzi wa miradi mingine ya maendeleo hususani afya ,Miundombinu na elimu lengo likiwa ni kuimarisha ustawi wa jamii za kitanzania .
Katika hatua nyingine katibu tawala ametoa rai kwa wakandarasi kuhakikisha wanakamilisha ujenzi ndani ya muda wa mkataba kwasababu kutofanya hivyo kutaendelea kuwakosesha huduma wananchi.
“Nikuombe mkandarasi unasimamia ujenzi wa jengo hili la makao makuu ya halmashauri ya wilaya ya Njombe uharakishe ujenzi ,ili serikali itoe fedha kwa ajili ya awamu ya pili na tatu,Alisema Judica Omary katibu tawala mkoa wa Njombe.
Kwa upande wake Joseph Mutashubila Muhandisi wa mkoa ,akitoa maoni kuhusu mradi wa zahanati ya Lole amesema ameridhishwa na ubora wake lakini kuna kasoro ndogo kwenye mifumo ya maji na vitasa na kisha kutoa agizo kufanya maboresho ili kuendana na viwango vya serikali.
“Nimependa ubora wa mradi huu wa zahanati lakini naomba yafanyike marekebisho madogo kwenye vitasa vya milango na mifumo ya maji kabla ya kufanya makabidhiano,Alisema Mutashubila.
Akitoa ufafanuzi kuhusu changamoto zilizobainika mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Njombe amesema amepokea maelekezo hayo na kwamba hata kabla ya kuagizwa alishabaini na kuanza kufanyia kazi huku pia akisema kinachokwamisha ni upungufu wa fedha zilizotolewa na TASAF kutekeleza mradi huo.
“Nimeshaandika maombi ya kuomba kuongezewa fedha na kupeleka makao makuu ya TASAF ili kuongezewa fedha kidogo za kumalizia mradi huu muhimu kwa wakazi wa kijiji hiki cha Lole,alisema mkurugenzi wa halamshauri ya wilaya ya Njombe Sharifa Nabarang’anya
Aidha mkandarasi anayejenga jengo la utawala la halmashauri ya mji wa Njombe mhandisi Athuman Kigolo kutoka MUST amesema yeye na timu yake wanafanya kila jitihada kukamilisha mradi huo kwa wakati licha ya kukabiliwa na changamoto ndogo ikiwemo ya kucheleweshwa kwa malipo na nguvu kazi ya vijana ambapo hulazimika kwenda mikoa ya kaskazini kutafuta wafanyakazi hatua ambayo ni matokeo ya wenyeji kujikita mashambani na kwenye biashara ya mbao.
Kutekelezwa kwa miradi hiyo inayogusa maisha ya watu wote katika jamii ,Kumeleta hisia kubwa kwa wananchi ambapo wananchi nao wameamua kuunga mkoano jitihada za serikali kwa kuchangia nguvu kazi kwa asilimia 20 ikiwa ni pamoja na kuchimba msingi,ulinzi wa mradi pamoja na kusogeza vifaa vya ujenzi.
“Kutokana na umuhimu wa miradi hii ,Serikali za vijiji na wananchi zimekubaliana kuweka utaratibu wa kuchangia nguvu kazi na kisha kuweka sheria na adhabu kwa ambaye atapuuza,alisema Afred Kaduma.