Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Chikongo kilichopo kata ya Mkoreha kwenye mkutano wake wa kusikiliza na kutatua kero za Wananchi
…………………….
Na Mwandishi wetu Mihambwe
Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu ameagiza Wananchi kurudishiwa fedha zao walizolazimishwa kutoa ili wapatiwe huduma za kupewa fomu, kugongewa muhuri na kusaidiwa kujaza fomu za kuomba kitambulisho cha Taifa.
Hayo yamejitokeza kwenye mkutano na Wanakijiji wa kijiji cha Chikongo kilichopo kata ya Mkoreha ambapo Wanakijiji hao walilalamika mbele ya Gavana Shilatu kutozwa fedha hizo kinyume na utaratibu na ambao waliokataa kutoa hawakupatiwa fomu ama huduma yeyote ile.
“Hakuna utaratibu wa fomu ya kuomba kitambulisho cha Taifa kulipiwa; ama kulipia kugongewa muhuri; au kuomba msaada wa kusaidiwa kujaza fomu mpaka utoe fedha Shilingi elfu moja, hakuna bali Mwananchi anatakiwa ahudumiwe bure. Naagiza ndani ya saa 24 Wananchi wote waliochukuliwa fedha zao kurudishiwa mara moja fedha zao, Mtendaji Kata na Mtendaji Kijiji simamieni utekelezaji wa agizo langu. Serikali inatoa huduma ya kuwapatia vitambulisho vya Taifa Wananchi bure kabisa na huduma iendelee kutolewa bure na pasisikike tena malalamiko ya Wananchi kutozwa fedha.” Alisisitiza Gavana Shilatu.
Katika mkutano huo walijitokeza Watu 18 na wengineo zaidi ambao hawakufika mkutanoni wakitajwa kuchukuliwa Shilingi elfu moja moja zao ili wapatiwe huduma, Gavana Shilatu ameagiza wote waliotozwa elfu moja warejeshewe fedha zao.
Wakizungumzia uamuzi wa Gavana Shilatu wamefurahishwa kuona fedha zao zinarudi na huduma kuagizwa itolewe bure kabisa.
“Sie tunajua huduma inatolewa bure na tulikuwa tunashangaa kuona tunatozwa fedha. Tunamshukuru Afisa Tarafa Mihambwe kuingilia Kati Mara moja tulivyomfikishia kero yetu hii. Tunafurahi kuona Viongozi wetu wanaposimama nasi Wananchi” alisema Mwanakijiji Ndevu.
Wakati huo huo Gavana Shilatu ametumia mkutano huo wa kusikiliza na kutatua kero za Wananchi kuwahamasisha Wananchi kujitokeza kwa wingi kuupokea Mwenge wa Uhuru 2019 utakao kuwa wilayani Oktoba 4; Pia Kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kupiga kura Novemba 24, 2019.
Mkutano huo ulihudhuliwa pia na Mtendaji Kata Mkoreha, Mtendaji Kijiji Chikongo, Mwenyekiti Kijiji Chikongo pamoja na Wajumbe Halmashauri ya Kijiji Chikongo na Wananchi.