*********************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MKUU wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Dkt Suleiman Hassan Serera amekemea ufujaji na ubadhirifu wa matumizi ya fedha mbichi kwenye vijiji na kata.
Fedha mbichi ni fedha taslimu zinazokusanywa na zinazotolewa benki kwa malengo ya kuhifadhiwa au kutumika kwa matumizi mbalimbali.
Dkt Serera akizungumza na watumishi wa serikali, maofisa tarafa, madiwani, watendaji wa vijiji na kata, wenyeviti wa vitongoji na vijiji amesema matumizi ya fedha mbichi yanapaswa kuwa ya uangalifu.
Amesema fedha zote zinazokusanywa na kutolewa benki kwenye vijiji na kata zote zinapaswa kutumika kwa malengo husika na siyo vinginevyo.
Ametoa onyo kwa wenyeviti wa vitongoji na vijiji kuwa waadilifu na kuwajibika ipasavyo kwani hata wakistaafu na ikiwa walifuja fedha watashtakiwa na kufungwa.
“Kuna mwenyekiti wa kijiji mstaafu ambaye aliuza ardhi na kufuja fedha akafikishwa mahakamani na kuhukumiwa miaka minne kwenda jela hivyo kuweni makini,” amesema Dkt Serera.
Mwenyekiti wa CCM wa wilaya ya Simanjiro Kiria Laizer amewataka wenyeviti wa vitongoji na vijiji kuwa waaminifu na kuondokana na uuzaji wa ardhi kiholela.
Kiria amesema chama hicho hakitamuonea huruma kiongozi yeyote atakayeuza ardhi na kusababisha migogoro ya ardhi.