Na John Walter-Manyara
Mtu mmoja aliefahamika kwa jina moja la Agustino mkazi wa Kijiji cha Hoshan kata ya Riroda wilayani Babati mkoani Manyara amefariki dunia baada ya kutumbukia kwenye andaki lenye maji wakati akijaribu kuchimba madini eneo la Mlima Huan akiwa na wenzake.
Mwenyekiti wa kijiji cha Hoshan Yoel Noga amesema tukio hilo limetokea Ijumaa na mwili wake kupatikana Jumatatu Oktoba 31 saa nne Usiku na kuwashtua wengi.
Mwenyekiti huyo amesema hakuna madini yoyote yaliyotambulika kwenye eneo hilo la Mlima Homam, ila watu hao walikuwa wakichimba kwa hisia shimo hilo ambalo lilikuwa limejaa maji ya mvua ya msim uliopita.
Aliyefariki aliitwa na wenzake ili akawasaidie kutoa nje maji hayo kwa kutumia Jenereta lake ambalo lilishindwa kufanya kazi na kusababisha moshi mkubwa uliowanyima pumzi wakiwa shimoni humo ambapo katika kujiokoa, Agustino alizidi kuzama kwenda chini zaidi huku wenzake ambao idadi yao kamili haijafamika wakifanikiwa kutoka.
Amesema walifanikiwa kuupata mwili huo baada ya Jeshi la zimamoto na uokoaji wakishirikiana na TANESCO kufanikiwa kuvuta maji yaliyokuwemo kwenye shimo hilo na kufanikiwa kuupata ukiwa chini kwenye kina kirefu.
Ameeleza kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya Babati Vijijini Jackson Haibey ndiye aliefanikisha hilo baada ya kuwasiliana na mkuu wa wilaya ambaye alituma waokoaji waliopambana kuanzia Jumamosi hadi Jumatatu usiku walipofanikiwa kuutoa mwili huo huku wengine waliokua naye wakikimbia.
Kamanda wa polisi mkoa wa Manyara George Katabazi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba wataongea na watu husika ili kuangalia utaratibu mzima wa uchimbaji madini upoje na kuzuia majanga hayo kutokea kwa sababu ni suala la maisha ya watu.