Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwasikiliza wadau mbalimbali kwenye mabanda ya maonesho kuhusu matumizi ya Nishati safi ya kupikia kabla ya kufungua Kongamano la Kitaifa kuhusu Nishati hiyo lililofanyika katika ukumbi wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.
………………………
Na Alex Sonna
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan ametangaza dira na mkakati wa miaka 10 ya kuhamia kwenye nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 20232.
Rais Samia ametangaza Mkakati huo wakati akifungua Kongamano la Kitaifa kuhusu Nishati hiyo lililofanyika katika ukumbi wa Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam.
Rais Samia amesema utaanza mwakani kwa serikali kutenga fedha za kutosha zitakazoanzisha mfuko wa nishati safi ya kupikia, lengo likiwa ni kumtua mama kuni kichwani.
“Ifikapo mwaka 2032 nataka asilimia 80 mpaka 90 ya Watanzania wawe tayari wanatumia nishati safi ya kupikia,” amesema Rais Samia.
Amemuagiza Waziri wa Nishati Januari Makamba kuhakikisha taasisi zote zinazohudumia watu zaidi ya 300 watumie nishati safi na sio mkaa kwa mwaka 2023.
“Ukiwa Wizara ya Mazingira nilikuelekeza, lakini kabla haujatekeleza ukaondoka, sasa nakuelekeza tena leo, taasisi zote kuanzia jela, mashule, vikosi vya ulinzi na usalama na taasisi nyingine zote zianze kujielekeza kwenye nishati safi, wanaweza kupelekewa gesi nakupa mwaka ujao wote, utekelezaji huo ufanyike.
“Stamico wazalishe kwa wingi mkaa ambao unatumia kidogo, mkaa safi basi utumike mkaa huo badala ya kukata miti hovyo, nataka ifikapo 2024 nisimame kwa wananchi niseme nimeweza kufanya hiki na kile,” amesisitiza
Kwa upande wake Waziri wa Nishati, January Makamba,amesema kuwa kongamano hilo linalenga kuwaokoa maelefu ya Watanzania ambao wamekuwa wakiathirika kutokana na kutumia nishati inayotokana na kuni, mkaa na mabaki ya mazao na vinyesi vya wanyama.
”Takwimu zinaonyesha kuwa, zaidi ya watu 30,000 wanapoteza maisha kila mwaka kutokana na kutumia nishati ya kuni na mkaa ambayo, kiafya sio salama lakini kutokana na changamoto mbalimbali imewalazimu kutumia.”amesema Waziri Makamba
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Felchesmi Mramba amesema kuwa mjadala huo ni safari ya awali ya kuhama kwenye nishati isiyo salama ya kupikia na kuelekea nishati safi ya kupikia .
“Tunatambua madhara yanayopatikana kwa kutumia nishati ya kupikia isiyo salama na inaleta madhara mbalimbali ikiwemo athari kiafya,kiuchumi,kijamii hivyo wadau na taasisi zitajadili namna ya taifa litahamia kwenye nishati safi ili kuepuka matatizo hayo”amesema
Awali Mbunge Mstaafu Prof. Anna Tibaijuka,ameiomba Serikali kuweka utaratibu mzuri wa kibiashara kwa wauzaji wa nishati ya gesi ili waweze kuyafikia maeneo mengi hasa ya vijijini.
“Mimi mwenyewe ni muhanga wa watu walikuwa wakikumbana na adha ya utafutaji kuni hivyo naelewa fika suala hili kama kweli mjadala huu unalenga kuleta unafuu ni wazi kwamba tunahitajika kuchukua hatua rafiki kwa kuwashirikisha Wafanyabiashara wa gesi,”