Na Mwandishi wetu, Kiteto
HALMASHAURI ya Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara, imejipanga kufanya harambee kubwa ya kupata fedha za ununuzi wa madawati ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa madawati kwenye shule za msingi Wilaya hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kiteto John John Nchimbi amesema harambee hiyo inatarajiwa kufanyika Novemba 2 mwaka 2022 kwenye uwanja wa mpira Kibaya.
Nchimbi amesema wana Kiteto wamejipanga kwa hali na mali kwenye harambee hiyo ya mpango mkakati wa kukabiliana na changamoto ya upungufu wa madawati katika shule za msingi.
“Bei ya dawati moja ni shilingi 80,000 mahitaji ya madawati kwenye shule za msingi Kiteto ni 21,069 yaliyopo ni madawati 12,046 upungufu ni 9,023,” amesema Nchimbi.
Amewakaribisha wadau wote wa maendeleo wa ndani na nje ya Kiteto katika kushiriki shughuli hiyo ya maendeleo ya kuchangia madawati ya wanafunzi wa shule za msingi Kiteto.
Katibu wa CCM wilaya ya Kiteto Denis Mwita amesema jamii na viongozi wajitoe kwa hali na mali ili kuondoa upungufu huo wa madawati na wanafunzi kusoma kwa kujinafasi.
“Jambo limeiva, ni wajibu wa wananchi wa Kiteto wakiongozwa na sisi viongozi wa kada mbalimbali kujitoa kwa hali na mali kuchangia madawati ya watoto wetu,” amesema Mwita.
Mkazi wa kijiji cha Partimbo James Leyani amesema Kiteto ina utajiri mkubwa wa mifugo na mashamba hivyo anategemea jamii itajitoa kwa wingi kuchangia madawati hayo.