Na John Walter-Manyara
Takwimu za kitaifa zinaonesha kuwa mwaka 2021 watoto waliofanyiwa ukatili ni 11,499 ambapo kati ya hivyo ubakaji ni 5899, huku waliopewa ujauzito ni 1677 na watoto waliolawitiwa ni 1114.
Naibu katibu mkuu wa wizara ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju, amesema kwa sasa serikali imejipanga vyema kwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuingia mikataba ya kitaifa na kikanda yenye maudhui ya kutokomeza ukatili na kusimamia katiba na sheria za watoto ili kuhakikisha wanakuwa salama.
Akizungumza kwenye mkutano wa kilele cha kampeni ya kutokomeza Ukeketaji Mkoa Wa Manyara uliofanyika katika kijiji cha Mandi kata ya Dabil Oktoba 12 2022,Mpanju amesema serikali imeunda mikakati ya kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto uliundwa mwaka 2017-2018 ambao umekamilika mwaka 2022.
Amesema kwa sasa serikali ipo kwenye tathmini ya kutambua wadau muhimu wa kupinga ukatili wakiwemo wananchi ambapo kila mmoja anapaswa kuwa sehemu ya kuzuia vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto.
Kwa upande wake katibu tawala mkoa wa Manyara Carolina Mthapula amesema lengo la mkoa wa manyara ni kumaliza vitendo vya ukatili ili kuuondoa mkoa wa Manyara kuwa moja kati ya mikoa vinara kwenye vitendo vya ukatili.
Carolina pia ameishukuru serikali kwa jitihada za kutokomeza ukatili ndani ya mkoa wa Manyara, kwani inatia moyo na chachu kwa viongozi katika kupambana na changamoto hiyo kwenye maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi waliojitokeza katika kilele cha maadhimisho ya kupinga ukatili wamesema angalau kwa sasa matukio ya ukatili yamepungua kwa kiasi kikubwa, hivyo wanaiomba jamii kuacha vitendo hivyo huku wakiiomba serikali kutia nguvu zaidi ili kuvitokomeza kabisa vitendo hivyo.