******************
Na Oscar Asaenga,TANGA
KITUO cha Sayansi cha Jijini Tanga ( STEM PARK TANGA) watazindua mradi wa kuangalia namna ya kuweza kuwafikia wanafunzi waliopo umbali wa kilomita tano ili kuhakikisha nao wananufaika na mafunzo ya sayansi kwa vitendo.
Hayo yalisemwa leo na Meneja wa Kituo cha Sayansi kilichopo eneo Kisosora Jijini Tanga Max George wakati akizungumza na Nipashe kuhusu namna walivyojipanga kuwafikia wanafunzi waliopo pembezoni kilomita 5 kutoka kwenye kituo hicho na Jiji laTanga.
Alisema kwamba wao watakuwa wakiwafuata shuleni ambapo mpango huo utaanza Novemba 5,2022 watatembelea shule zote na kuwafikia wanafunzi 800 kwa kipindi cha wiki nne na watakuwa wakienda kila Jumamosi.
Alisema kwamba kupitia mpango huo wanaamini utawasaidia wanafunzi wengi wenye ndoto za kusoma masomo ya sayansi kwa vitendo na hivyo kuongeza wataalamu kupitia fani hiyo siku zinazo.
” Lengo letu hili ni kuhakikisha wanafunzi wanaokaa umbali wa Kilomita 5 kutoka eneo la Kituo nao tuweze kuwafikia lakini pia namna ya kuzifikia na shule za binafsi na tumetembelea shule 20 mpaka sasa”Alisema.
Aidha alisema kwamba katika kituo hicho wamekuwa wakihakikisha wanafunzi wanasoma masomo ya sayansi kwa vitendo ambapo wanafanya kazi moja kwa moja walimu na maafisa kwa kuangalia namna ambao unarahisisha ufundishaji walimu kwa kutoa namna mbalimbali ufundishaji wa masomo hayo unakuwa rahisi.
“Watawasaidia walimu na wanafunzi namna mtaala unavyohitaji kwa kuanzisha mfumo ambao walimu na wataalamu wa kituo cha sayansi tunamuandalia mazoezi kwa vitendo ili kumrahisishia anapomaliza inakuwa ni rahisi watoto kuelewa wanachofundishwa na inakwenda ngazi ya msingi mpaka sekondari”Alisema.
Hata hivyo alisema mfumo huo waliouanzisha unawezesha watoto kuanza kupenda masomo ya sayansi kabla hata ya kuanza kutumia maabara na hivyo kuweza kujifunza kwa tija na mafanikio makubwa.