Na.Joctan Agustino-NJOMBE
Bodi ya filamu nchini imetoa rai kwa watayarishaji wa filamu mkoani Njombe kutumia fursa ya kipekee ya utajiri wa vivutio kutengeneza filamu zenye maudhui za utalii ili kutengeneza fedha nyingi kutoka ndani na nje ya nchi.
Rai hiyo imetolewa na Benson Mkenda kaimu meneja wa kitengo cha utayarishaji bodi ya filamu Tanzania akiwa mkoani humo wakati wa zoezi la kukusanya filamu mtaa kwa mtaa kwa watayarishaji wadogo na wakubwa huku lengo likiwa ni kuzingiza kwenye kinyang’anyiro cha kuwania tuzo za filamu zinazotarajiwa kutolewa mwishoni mwa mwaka huu.
Mkenda amesema wakati umefika kwa watayarishaji wa filamu nchini kuchangamkia fursa ya uwepo wa vivutio vingi vya utalii ikiwemo Milima,Bahari,Mapango ya kihistoria na vinginr vingi kuandaa filamu za tofauti ambazo zitavutia wageni kuja nchini kutembea.
Kwa mujibu bodi ya filamu inaelezwa takribani vibali 160 hutolewa kila mwaka kwa watayarishaji wa kigeni kuja nchini kutayarisha filamu katika maeneo tofauti ya vivutio na kwamba kitendo cha kupata filamu 10 katika mkoa wa Lindi,Mtwara 21 na Ruvuma 25 kimeonyesha mwamko umeanza kukua katika tasnia hiyo.
“Tunapita mtaa kwa mtaa kukusanya filamu kutoka kwa watayarishaji na kisha kuziingiza kwenye kinyang’anyiro cha tuzo ,hatua ambayo itasaidia kuongeza hamasa kwa wazalishaji kuongeza bidii na ubunifu,Alisema Benson Mkenda kaimu meneja wa kitengo cha utayarishaji bodi ya filamu Tanzania”
Kwa upande wao baadhi ya wasanii waliyojitokeza katika mkoa wa Njombe kuwasirisha filamu zao katika bodi ya filamu ili ziingie kwenye mchujo akiwemo Happy Mwesi alimaarufu Angle Kidoti wanasema kitendo kilichofanywa na wizara kupitia bodi ya filamu kwasasa kimewapa ari ya kuongeza ubunifu ili kuzalisha maudhui bora na yatakayokidhi mahitaji ya dunia.
Wamesema hapo mwanzo walikuwa wanapata shida kuzifikia mamlaka kwa kulazimika kupanda gari hadi Dar es salaam lakini kitendo cha kufuatwa mitaani kinawapa nguvu.
Wakizungumzia kuhusu changamoto zilizokuwa zikikwamisha maendeleo ya tasnia ya filamu kipindi cha nyuma ni ushirikiano mdogo kutoka mamlaka za serikali ikiwemo bodi ya filamu lakini kinachofanywa sasa kinawafanya kutayarisha kuja kufanya mageuzi makubwa .