Na.Imani Kelvin Mbaga,Dar es Salaam
Si jambo rahisi sana kuzungumzia mambo ya miaka mingi ijayo, kana kwamba yameshakuwa au yamekaribia.
Dunia nzima inazungumzia Qatar 2022? Unaweza kuonekana mwehu kuzungumzia 2026 wakati wenzio wapo makini kujiandaa na 2022.
Lakini katika yote hayo najiuliza je? Tunataka kujiweka kundi moja na Morocco, Senegal, Brazil, Saudi Arabia, Korea kusini, Ufaransa, Hispania nk? Kwamba kwa kuwa wao wanazungumzia Qatar basi nasi tujiingize kwenye mjadala huo?
Ni vema tukawa “wehu” kwa sasa hivi, tukiwaacha wao waendelee, kujiandaa na kupigania nafasi na sisi tuwekeze nguvu zetu zote kwenye kufuzu 2026.
Tunaweza kufanya hivyo kwakuwa mtaji wa kufanya hivyo tunao na tukiamua “kudunduliza” sasa nina uhakika ifikapo 2026 tutakuwa miongoni mwa watu watakaokuwa wametulia wanakula “popcon” kusubiria kipyenga cha kuanza kwa michuano hiyo kama washindani na si wasindikizaji au watazamaji.
Serengeti boys, Ngorongoro heroes na Karume boys ndiyo mtaji wetu kwa sasa.
Tunahitaji serikali kupitia wizara, baraza la michezo na shirikisho la soka kwa upande mmoja, na wadau wote wapenda soka kwa upande mwingine tukae chini tuwaze na kuja na jibu moja muafaka la kufanya mapinduzi makubwa ya mfumo wa uendeshaji soka nchini kwetu.
Badala ya kuwaahidi hawa vijana mamilioni ya fedha endapo watafanya vzr kwenye michuano fulani, tuamue kuwa zawadi pekee ni kuwapeleka na kuwalipia shule za soka huko barani ulaya kwenye nchi angalau tatu tofauti.
Ungeniambia nichague ningesema Ureno, Ufaransa na Uholanzi ambako pamoja na kufundishwa soka kitaalamu pia ingekuwa ni rahisi kwa wao kupata mawakala timu za kuchezea wawapo kwenye shule hizo, wakati huo huo tungekuwa tunawatumia kama timu ya taifa ya vijana ambayo tungeipa majukumu ya kufuzu kwa AFCON NA KOMBE LA DUNIA kwa vijana U’17 na U’20.
Wakati haya yakiendelea tungeingia mkataba na moja ya vyama vya soka huko barani ulaya pamoja na UEFA kwa msaada wa FIFA kutufundishia waalimu wa soka “makocha” kwa VIWANGO mbalimbali ambao wangekuja kutufundishia vijana wetu katika shule za msingi na sekondari.
Kama serikali ikiweza kuajiri mwalimu mmoja kila shule, au kuwafundisha masomo ya “ukocha” waalimu wote wa michezo wa shule za msingi na sekondari angalau kwa kiwango cha cheti na stashahada basi maana yake Kwa miaka 7 tuna uwezo wa kuzalisha wachezaji zaidi ya elfu tano waliokulia katika misingi sahihi ya soka ambao wanaingia katika ngazi ya soka la ushindani.
Tunapofanya haya ni muhimu kutambua kuwa hakuna njia ya mkato kufikia mafanikio katika soka.
Tuanze sasa safari ya kombe la dunia 2026 na inawezekana.
Wakati wenzetu wana akina Samatta na Msuva kwa maelfu sisi hatuna mpango wa kuzalisha wengine kwa uwingi huku tukisubiri kudra za Mwenyezi ili kufuzu kwa michuano mikubwa ya kimataifa.
Wasaalamu