Mlinzi wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) UVCCM (Green Guard) Ramadhan Ramadhan Hamis baada ya kudaiwa kujeruhiwa mkononi na mbunge huyo.
************************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
SAKATA la Mbunge wa Jimbo la Simanjiro Mkoani Manyara, Christopher Ole Sendeka kudaiwa kumjeruhi mlinzi wa Jumuiya ya Umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi UVCCM (Green Guard) Ramadhan Ramadhan Hamis, bado polisi wanaendelea nalo.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi (ACP) George Katabazi amesema bado wanaendelea na uchunguzi wa jalada la mbunge huyo Ole Sendeka.
Kamanda Katabazi amesema wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo la Ole Sendeka la shambulio la kudhuru mwili ili wapeleke jalada kwa wakili wa serikali kwa hatua nyingine za kisheria.
Katabazi amesema wakishakamilisha uchunguzi wa tuhuma hizo watalipeleka jalada la upelelezi wao kwa wakili wa serikali kwa hatua nyingine.
“Bado tunaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na endapo upelelezi ukikamilika tutafikisha jalada hilo kwa wakili wa serikali,” amesema Kamanda Katabazi.
Akizungumzia tukio hilo Ramadhan Ramadhan Hamis amesema alijeruhiwa na Ole Sendeka kwenye uchaguzi wa jumuiya ya wanawake UWT Oktoba 15 wakati akiwaita wajumbe ili washiriki kwenye uchaguzi huo.
Ramadhan amesema alifanyiwa tukio hilo wakati akiwaita baadhi ya wajumbe hao ili waende kwenye ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro uliokuwa unafanyika uchaguzi huo.
Amesema ni mara nyingi Ole Sendeka amekuwa akimtishia kuwa atamuonyesha dawa yake kwani alianza ugomvi naye kwenye baadhi ya chaguzi za jumuiya yeye akiwa mlinzi.
“Alidhani nilikuwa nampiga picha kwa kutumia simu akiwa na baadhi ya wajumbe wa uchaguzi huo wa UWT ndipo akanikamata na kunisukumia kwenye gari na kunijeruhi mkononi,” amesema.
Amesema baada ya kumshambulia na kumjeruhi alimtolea bastola na kumkandamiza nayo tumboni huku akimfinyia kwenye mbavu.
Hata hivyo, Ole Sendeka amekanusha kumjeruhi kijana huyo mlinzi wa CCM akidai kuwa tukio hilo limetengenezwa na maadui wake wa kisiasa kwani hakumpiga wala kumjeruhi.
“Umeona wapi mtu akapigwa na kuumizwa kidole pekee? mimi sikumpiga huyo kijana wa UVCCM ni tuhuma tuu za kutunga zilizopangwa na maadui wangu wa kisiasa,” amesema Ole Sendeka.
Akizungumzia tuhuma za kutoa rushwa na kupigwa picha kwenye uchaguzi huo wa UWT, Ole Sendeka amekanusha na kudai kuwa hakuwa akitoa rushwa kwa mjumbe yoyote.
“Hakukuwa na rushwa yoyote iliyotolewa na mimi kwani nilikuwa pembeni ya gari langu sikuwa natoa rushwa kwa mjumbe wa uchaguzi huo zaidi ya kuongea na baadhi ya madiwani,” amesema Ole Sendeka.
Diwani wa kata ya Ngorika Albert Msole ameaani vikali tukio hilo kwa kudai kuwa kiongozi anayethubutu kumpiga ua kumjeruhi kijana wa UVCCM atakuwa hajitambui.
“Vijana mnapaswa kulaani tukio hilo kwani vijana tunawategemea kwenye kuimarisha ulinzi wa CCM ila anapotokea kiongozi mmoja na kumjeruhi mwenzenu msinyamazie hilo,” amesema Msole.