Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji cha Mpanga wilayani Wanging’ombe wakati Kamati ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta ilipotembelea kijiji hicho mkoani Njombe Oktoba 27, 2022′
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (kushoto), Naibu Waziri Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega (wa pili kushoto) na Naibu Waziri Maliasili na Utalii Mery Masanja wakicheza na bibi aliyekuwa akifurahia maamuzi ya serikali kukibakisha kijiji cha Mpanga kilichokuwa kwenye hifadhi ya Mpanga Kipengele wakati Kamati ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta ilipotembelea kijiji hicho mkoani Njombe Oktoba 27, 2022′
Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde (katikati) na Mkuu wa Mkoa wa Njombe Anthony Mtaka (kulia) wakimsiliza Bi Neema (kushoto) ambaye ni mkulima wa mahindi na mkazi wa kijiji cha Mpanga wilaya ya Wanging’ombe wakati Kamati ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta ilipotembelea kijiji hicho mkoani Njombe Oktoba 27, 2022′
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega akisisitiza jambo mbele ya Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula na Mkuu wa mkoa wa Njombe Anthony Mtaka wakati Kamati ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta ilipowasili ofisi ya Mkuu wa mkoa Njombe Oktoba 27, 2022 (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
************************
Na Munir Shemweta, WANMM NJOMBE
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ametaka maeneo ya yanayomegwa kwa ajili ya kupatiwa wananchi waliovamia hifadhi yapangiwe mpango wa matumizi ya ardhi na kutolewa hati kwa wamiliki wake.
Dkt mabula alitoa kauli hiyo oktoba 27, 2022 katika kijiji cha Mpanga kilichopo wilaya ya Wanging’ombe wakati timu ya mawaziri nane wa wizara za kisekta inayoshughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 ilipotembelea mkoa wa Njombe ikiwa ni mfululizo wa ziara zake kawenye mikoa ya Tanzania Bara.
Kijiji cha Mpanga ni moja ya vijiji 11 vilivyopo wilaya ya Wanging’ombe na Makete mkoani Njombe ambavyo vimemegewa eneo kutoka hifadhi ya Pori la Akiba la Mpanga Kipengele.
Dkt Mabula alisema, serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeridhia baadhi ya vijiji kwenye mkoa wa Njombe kubaki maeneo ya hifadhi za Mapori ya Akiba ingawa wananchi wake waliingia bila ridhaa ya serikali.
Kwa mujibu wa Dkt Mabula, ili kuondokana na migogoro ya ardhi vijiji vilivyomegewa maeneo vitapimwa na kumilikishwa ili wamiliki kujua mipaka sambamba na kuweza kutumia hati kukopa fedha benki na fedha kutumika kuboresha shamba au mifugo.
“Kinachofanyika hapa siyo tu kutoa maeneo, eneo linatolewa lakini liwekewe mpango mzuri na endelevu ili kuona jinsi gani mnaweza kutumia ardhi mliyopewa kwa faida na kwa sababu tunaongezeka basi mpango uwe mzuri na endelevu” alisema Dkt Mabula.
Amebainisha kuwa, ni lazima maeneo yanayopangwa yaanishwe matumizi yake kama vile maeneo ya akiba, hifadhi, makazi na uwekezaji na kutaka wakati wa utekelezaji wataalamu wazingatie mpango wa matumizi katika maeneo hayo.
Timu ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta ambayo inashughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi kwenye vijiji 975 imemaliza ziara yake katika mkoa wa Njombe ukiwa ni mkoa wa 22 kati ya 26 ya Tanzania Bara na inaendelea na ziara yake katika mkoa wa Ruvuma.