Katibu,Ofisi ya Rais,Tume ya Utumishi wa Walimu Mwalimu Paulina Nkwama ,akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali ya tume hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023 leo Oktoba 27,2022 jijini Dodoma.
…………………………………
Na Alex Sonna-DODOMA
TUME ya Utumishi wa Walimu (TSC),imewachukuliwa hatua za kinidhamu walimu 1952,wenye makosa mbalimbali ikiwemo walimu 119 kwa kosa la mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi kuanzia Machi 2021 hadi Septemba 2022.
Aidha,imetoa adhabu mbalimbali kwa walimu waliofanya makosa ikiwemo kuwafukuza kazi walimu 1,642.
Hayo yamesemwa leo Oktoba 27,2022 jijini Dodoma na Katibu,Ofisi ya Rais,Tume ya Utumishi wa Walimu Mwalimu Paulina Nkwama ,wakati akitoa taarifa kuhusu Utekelezaji wa Shughuli mbalimbali ya tume hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Mwl.Nkwama amesema kuwa katika mashauri 1,642 yaliyoamuliwa,Walimu 919 sawa na asilimia 56 ya adhabu zilizotelewa walifukuzwa kazi, Walimu 234 sawa na asilimia 14.3 hawakupatikana na hatia, Walimu 115 sawa na asilimia 7 ya adhabu zilizotolewa walishushwa cheo, Walimu 89 sawa na asilimia 5.4 walikatwa mshahara asilimia 15 kwa muda wa miaka mitatu na Wengine 143 sawa na asilimia 8.7 walipewa adhabu ya Karipio.
“Katika mashauri 1,642 yaliyoamuliwa Walimu 919 sawa na asilimia 56 ya adhabu zilizotelewa walifukuzwa kazi, Walimu 234 sawa na asilimia 14.3 hawakupatikana na hatia, Walimu 115 sawa na asilimia 7 ya adhabu zilizotolewa walishushwa cheo, Walimu 89 sawa na asilimia 5.4 walikatwa mshahara asilimia 15 kwa muda wa miaka mitatu na Walimu 143 sawa na asilimia 8.7 walipewa adhabu ya Karipio.”Ameeleza Mwl.Nkwama
Aidha Mwl.Nkwama amesema ,katika kipindi cha miaka mitatu kwa fedha (2020/2021) shilingi Bilioni 14.773 zilitengwa kwenye bajeti huku (2021/2022) iliongezeka hadi kufikia billion 14.980 ambapo (2022/2023) bajeti ya tume hiyo iliendelea kuongezeka zaidi na kufikia kiasi bilioni 15.454 ikiwa ni kutokana na juhudi za serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.
“Katika kipindi cha miaka mitatu (2020/2021; 2021/2023; 2022/2023) mfululizo Bajeti ya Tume imeendelea kuongezeka kutoka shilingi Bilioni 14.773 , 14.980 na 15.454 sawia. Hii ni kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya awamu y a sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”.
Akielezea mafanikio yaliyopatikana tangu Serikali ya awamu ya sita kuingia madarakani katika kipindi cha kuanzia mwezi Machi, 2021 hadi mwezi Septemba, 2022; Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameiwezesha TSC kufanikiwa kutekeleza majukumu mbalimbali ambayo yameendelea kuboresha mazingira ya Walimu na Sekta ya Elimu kwa ujumla.
“Tangu serikali hii ya awamu sita iingie madaraka Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na Walimu 16,749 kuajiriwa,wakiwemo 8,949 wa Shule za Msingi na 7,800wa Shule za Sekondari,Jumla ya Walimu 15,802 walisajiliwa, Walimu wa Shule za Msingi walikuwa 8,512na Sekondari walikuwa 7,290 wakati Walimu 6,949 sawa na asilimia 100 walithibitishwa kazini wakiwemo 3,949 wa Shule za Msingi na 3,000 wa Shule za Sekondari,”Ameeleza Mwl.Nkwama
Mwl.Nkwama Tume imekuwa ikishughulikia changamoto ya mwalimu mmoja mmoja kwa wale ambao wamekuwa wakilalamika kucheleweshwa kupandishwa madaraja miaka iliyopita ili kuhakikisha kwamba kila mwalimu anapata anachostahili.
Ameelezea kuwa zoezi hili hufanywa kwa kushirikiana na waajiri (Wakurugenzi wa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa) na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
“Jumla ya Walimu 47,158 walipandishwa cheo (Walimu 22,943 ni wa Shule za Msingi na 11,524 wa Sekondari kwa mwaka 2021/2022). Aidha kwa mwaka 2020/2021 walimu walipandishwa cheo ni 126,346,”Amesema Mwl.Nkwama
Katika hatua nyingine Mwl. Nkwama ameeleza kuwaTume hiyo imeweza kuwajengea uwezo Watumishi 58 kwa kuwawezesha kuhudhuria mafunzo ya muda mrefu na mfupi ambapo Watumishi watano (5) wanahudhuria mafunzo ya muda mrefu na mafunzo ya muda mfupi kwa kada saidizi (Watumishi 41) katika masuala ya utunzaji wa kumbukumbu, huduma kwa mteja na usalama mahala pa kazi.
“Aidha, Watumishi 12 walihudhuria mafunzo ya muda mfupi ya kitaaluma huku Mafunzo haya yote kwa ujumla wake yamegharimu jumla ya Shilingi 175,350,000.00”.Amesema Mwl.Nkwama
Na kuongeza kuwa “juhudi hizi za Serikali ya awamu ya sita zina lengo la kuiwezesha Tume ya utumishi wa walimu kuwahudumia Walimu kwa weledi na kuteta ufanisi zaidi katika kazi ya kuwahudumia walimu,”Amesema Mwl.Nkwama
Hata hivyo Tume hiyo inayohudumia jumla ya Walimu 266,388 Tanzania Bara, wakiwemo 177,956 wa Shule za Msingi na 88,432 wa Shule za Sekondari imesema itaendelea kusimamia Utumishi na Maendeleo ya Walimu kwa kudumisha Maadili na Nidhamu kwa Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari katika Utumishi wa Umma na itahakikisha Walimu wenye sifa ya kupandishwa vyeo na kubadilishiwa kazi wanapata huduma hiyo kwa wakati baada ya kibali kutolewa na Mamlaka husika.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari Maelezo Zamaradi Kawawa amesema serikali ya awamu ya sita imefanya mambo mengi katika kuboresha sekta ya elimu kama Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),ilivyoelekeza..